TAKUKURU yarejesha Sh milioni 1.2 za mradi wa shule

MANYARA: TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara, kupitia Ofisi ya Wilaya ya Simanjiro, imesaidia kurejesha Sh milioni 1.2 zilizokuwa sehemu ya fedha za ujenzi wa madarasa matatu na matundu sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Namalulu.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Anthony Gang’olo, amesema hayo leo Novemba 3, 2026, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026.

Amesema ufuatiliaji wa utekelezaji wa mradi huo ulibaini kuwa marumaru box 26 zenye thamani ya Sh milioni 1 na ‘skirting box’ sita zenye thamani ya Sh 244,062 hazikuonekana katika stoo, licha ya kuwepo kwa nyaraka za manunuzi, ikiwemo tax invoice na store ledger, zilizoonesha kuwa vifaa hivyo vilinunuliwa.

Gang’olo amesema Mtendaji wa Kijiji cha Namalulu, ambaye alikuwa msimamizi mkuu wa miradi hiyo, kwa kushirikiana na Mkuu wa Shule ya Msingi Namalulu, walieleza kuwa vifaa hivyo vilikuwa vimeibwa na wakaomba kurejesha fedha zilizotumika kuvipata.

Aidha, amesema TAKUKURU imefanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha katika miradi 10 ya maendeleo yenye thamani ya Sh 2,831,279,108.75 mkoani Manyara.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button