ACT Wazalendo kufanya ziara mikoa minane Bara

DAR ES SALAAM: Chama cha ACT Wazalendo kinatarajia kuanza ziara ya mikutano ya hadhara yenye takribani siku 20 itakayoanza Novemba 01, 2026 na kufikia mikoa 8 ya Tanzania Bara.

Ziara hiyo imepangwa kutembelea mikoa ya kanda ya ziwa, mikoa ya magharibi mwa nchi na baadhi ya mikoa ya nyanda za juu kusini.

Ziara hiyo itahusisha Viongozi wa Kitaifa wa Chama wakiongozwa na Kiongozi wa Chama Ndg. Dorothy Semu, Makamu Mwenyekiti Bara ambaye pia ni Waziri Mkuu Kivuli wa Baraza Kivuli la Mawaziri la ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita na Naibu Waziri Mkuu Kivuli na ambaye alikuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Luhaga Mpina.

Msafara wa ziara utagawanyika katika misafara miwili, ambapo msafara wa kwanza utakaongozwa na Kiongozi wa Chama na utaelekea mikoa ya Kigoma, Rukwa, Mbeya na Morogoro ukilenga kufikia Kata zenye Madiwani wanaotokana na ACT Wazalendo katika mikoa hiyo.

Kwa upande wake msafara wa pili, utaongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara akiambatana na Luhaga Mpina na utatembelea na kufanya mikutano ya hadhara kwenye mikoa ya Simiyu, mkoa wa kichama Kahama, mkoa wa Geita na mkoa wa Kagera.

Katika ziara hiyo, viongozi watazunguza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili. Aidha, masuala na ajenda mbalimbali za kitaifa zinazowahusu wananchi zitapata nafasi ya kuzungumzwa na kupewa uzito katika ziara hiyo.

Ajenda ya Uwajibikaji wa Serikali kufuatia mauaji ya wananchi ya Oktoba 29, 2025 na ufisadi mkubwa ulioibuliwa katika ripoti mbalimbali za CAG zitakuwa sehemu za ajenda muhimu zitakazotawala mazungumzo ya hotuba za viongozi katika ziara hiyo. Vilevile, chama kitatumia fursa ya ziara hii kupima na kutathmini uwajibikaji wa Serikali ya CCM katika utatuzi wa kero za wananchi katika maeneo yao.

Mbali na viongozi wakuu wa Chama watakaoongoza ziara hiyo, viongozi wengine mbalimbali nao wataambatana katika ziara hiyo wakiwemo Wajumbe wa Sekretarieti, Viongozi wa Ngome za Vijana na Wanawake, pamoja na Mawaziri na Manaibu Waziri Vivuli wa ACT Wazalendo.

Tunatoa wito kwa wananchi kote nchini kufuatilia kwa karibu ziara hii muhimu inayotarajiwa kuibua na kuzungumzia masuala yenye mguso na maslahi mapana ya umma.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button