Serikali yataka tafiti zenye tija kwa wafugaji

IRINGA:SERIKALI imetaka tafiti za kisayansi, teknolojia na ubunifu kutumika kuongeza tija katika sekta ya mifugo na uvuvi, huku matokeo yake yakilenga kutatua changamoto za wafugaji na kuboresha maisha yao.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dk Bashiru Ally Kakurwa, alitoa wito huo wakati akifungua Kongamano la 49 la Kitaaluma na Mkutano Mkuu wa 50 wa Chama cha Wataalamu wa Mifugo Tanzania (TSAP), mjini Iringa, leo Oktoba 28, 2026.

Alisema Tanzania inalenga kufikia utoshelevu wa protini inayotokana na nyama, maziwa, mayai na samaki kabla ya mwaka 2050, hivyo ni muhimu kuimarisha uzalishaji, ubora wa bidhaa na upatikanaji wa masoko ya uhakika.

Aliwataka wataalamu kuhakikisha matokeo ya tafiti yanawafikia wafugaji na kuwasaidia kuboresha afya ya mifugo, lishe, upatikanaji wa malisho na mbinu za uzalishaji, huku wakijiandaa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wa wafugaji, mafanikio ya tafiti yanapaswa kuonekana katika upatikanaji wa huduma za mifugo kwa wakati, gharama nafuu za matibabu na malisho, mifugo yenye uzalishaji mkubwa na masoko yenye bei zinazowanufaisha wazalishaji.

Changamoto nyingine zinazohitaji ufumbuzi ni magonjwa ya mifugo, uhaba wa malisho wakati wa kiangazi, gharama za pembejeo na upatikanaji wa teknolojia zinazoweza kutumiwa na wafugaji wadogo.

Hivyo, usambazaji wa elimu na matokeo ya tafiti unapaswa kwenda sambamba na uwezo wa wafugaji kuyatumia kwa vitendo.

Mwenyekiti wa TSAP, Dk Zabron Nziku, aliiomba Serikali kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na chama hicho ili kuunganisha tafiti, sera na teknolojia katika kutatua changamoto za sekta.

Alisema chama hicho chenye takribani wanachama 1,000 kimefikia asilimia 85 ya maandalizi ya kuanzisha jarida lake la kisayansi.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, alisema tafiti zinapaswa kutoa suluhisho la changamoto za wafugaji badala ya kuishia kwenye maandiko, akisisitiza umuhimu wa kupata mifugo bora na kuongeza uzalishaji.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Fabian Madele, alisema Serikali iko tayari kushirikiana na wataalamu kuendeleza tafiti na ubunifu unaoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Naye Mkurugenzi wa ASAS, Fuad Abri, alisisitiza umuhimu wa tafiti katika kuongeza ushindani wa bidhaa za mifugo, huku mtafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Gilbart Msuta, akitaka matokeo ya tafiti yawafikie wafugaji na kutumika kuongeza tija.

Kongamano hilo limefanyika chini ya kaulimbiu isemayo, “Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na Ujasiriamali kwa Minyororo Endelevu ya Thamani ya Mifugo na Samaki.”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button