Asilimia 85 wafaulu darasa la saba

DAR ES SALAAM: Jumla ya watahiniwa 970,876 sawa na asilimia 85.22 ya watahiniwa 1,139,273 waliofanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi mwaka 2026 wamefaulu kwa kupata madaraja ya A, B na C.

Akitangaza matokeo hayo leo Novemba 3, 2026 jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohamed, amesema takwimu hizo zinaonesha ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 3.42 ikilinganishwa na mwaka 2025, ambapo asilimia 81.80 ya watahiniwa walifaulu.

Amesema kwa kuzingatia jinsia, wavulana 443,254 sawa na asilimia 86.18 wamefaulu, huku wasichana 527,622 sawa na asilimia 84.43 wakifaulu.

“Mwaka 2025, ufaulu kwa wasichana ulikuwa asilimia 81.21, huku wavulana ukiwa asilimia 82.51. Hivyo, ufaulu wa wasichana umeongezeka kwa asilimia 3.22, wakati ufaulu wa wavulana umeongezeka kwa asilimia 3.67,” amesema.

Kwa upande wa ubora wa ufaulu, watahiniwa 429,667 sawa na asilimia 37.72 wamepata madaraja ya A na B, ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.82 ikilinganishwa na mwaka 2025.

Ubora wa ufaulu kwa wasichana umeongezeka kwa asilimia 0.56, kutoka asilimia 33.71 mwaka 2025 hadi asilimia 34.27 mwaka 2026.

Kwa wavulana, ubora wa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 1.17, kutoka asilimia 40.73 mwaka 2025 hadi asilimia 41.90 mwaka 2026.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button