Netanyahu apata pigo

ISRAEL: Tume ya Uchaguzi nchini Israel imethibitisha matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa Bunge uliofanyika wiki iliyopita, ambao uliondoa wingi wa viti wa muungano wa vyama vya mrengo mkali wa kulia unaoongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, huku ikikataa madai ya kuwepo kwa udanganyifu wa kura yaliyotolewa na waziri mkuu huyo.
Mpinzani mkuu wa Netanyahu, Gadi Eisenkot, amesema Netanyahu ameanzisha kile alichokiita “mashambulizi dhidi ya demokrasia” kwa kujaribu kubaki madarakani kupitia kudhoofisha uhalali wa kura zilizopigwa na kutumia vyombo vya usalama dhidi ya vyama vinavyoongozwa na raia wa Palestina nchini Israel.
Saa chache kabla ya tangazo hilo, Mwanasheria Mkuu wa Israel, Gali Baharav-Miara, alisema amekataa ombi la Idara ya Usalama wa Ndani (Shin Bet) la kuwahoji wanasiasa wakuu kutoka vyama vinavyoongozwa na Wapalestina, akieleza kuwa hakupewa ushahidi wowote wa makosa yanayodaiwa kufanywa.
Kwa mujibu wa NBC News, na Washington Post Baharav-Miara amesema katika nchi inayofuata utawala wa sheria, wananchi wala viongozi waliochaguliwa hawawezi kuhojiwa bila ushahidi unaohalalisha hatua hiyo.
Mamlaka za uchaguzi zimekabidhi matokeo rasmi kwa Rais wa Israel, Isaac Herzog, baada ya kuyathibitisha na kukataa madai kwamba uchaguzi huo uliathiriwa na uingiliaji mkubwa kutoka mataifa ya nje pamoja na udanganyifu wa kura.
Katika taarifa yake, Tume ya Uchaguzi imesema uchunguzi uliofanywa haukubaini ushahidi wa ukiukwaji wa taratibu ulioathiri uadilifu wa uchaguzi au matokeo yake.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Noam Sohlberg, amesema baadhi ya tuhuma bado zinafanyiwa uchunguzi, lakini hazina uzito wa kutilia shaka uhalali wa uchaguzi mzima wala kuhalalisha kucheleweshwa kwa kutangazwa kwa matokeo.
Akizungumza wakati wa kupokea matokeo hayo, Rais Herzog amelaani kauli za kibaguzi dhidi ya raia wa Kipalestina nchini Israel walioshiriki kupiga kura kwa idadi kubwa kihistoria.
Amesema analaani lugha za kibaguzi na kauli zisizo na staha zilizotolewa hivi karibuni, akisisitiza kuwa anaiheshimu jamii ya Waarabu nchini Israel na kutambua mchango wake katika maendeleo ya nchi hiyo.
Herzog ana nafasi muhimu katika mchakato wa kuunda Serikali mpya kwa kuwa ndiye atakayemteua mwanasiasa atakayepewa nafasi ya kwanza kuunda muungano wa vyama vya kuongoza nchi.
Eisenkot anatarajiwa kupewa jukumu hilo kutokana na kuungwa mkono na vyama vyote vya upinzani vinavyowakilisha jamii ya Wayahudi nchini Israel. Vyama vinavyoongozwa na Wapalestina navyo vimeeleza kuwa kipaumbele chao ni kuondolewa kwa Netanyahu madarakani, hivyo vinatarajiwa kumuunga mkono Eisenkot kama mgombea mwenye nafasi ya kufanikisha lengo hilo.
Hata hivyo, mazungumzo ya kuunda Serikali yanaweza kuchukua wiki kadhaa, huku Eisenkot akionya kuhusu juhudi zinazoendelea za kudhoofisha imani ya wananchi katika matokeo ya uchaguzi.
Amemtuhumu Netanyahu kutumia vyombo vya usalama dhidi ya wapinzani wa ndani kwa maslahi ya kisiasa ili kuendelea kubaki madarakani.



