Mwigulu ataka sera za viwanda zitekelezwe kwa vitendo

DODOMA: Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amezindua Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Ndogo na wa Kati, huku akizitaka taasisi za Serikali kuongoza kwa vitendo katika matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
Akizungumza leo Novemba 4, 2026, jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi wa sera hizo, Dk. Mwigulu amesema matumizi ya bidhaa za ndani yatasaidia kukuza viwanda, kulinda ajira, kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha uchumi wa Taifa.
Amesema Serikali inapaswa kuanza kwa kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini katika miradi yake ya ujenzi na ununuzi wa samani, badala ya kutegemea bidhaa kutoka nje wakati bidhaa hizo zinapatikana ndani ya nchi.
Amezitaja bidhaa hizo kuwa ni pamoja na vioo, nondo, marumaru na samani, akisisitiza kuwa taasisi za umma zinapaswa kuwa mfano katika kuunga mkono viwanda vya ndani.
“Jambo hili lianzie serikalini kwa kuwa Serikali inajenga majengo, hivyo bidhaa zinazozalishwa hapa nchini zitumike hapa nchini,” amesema.
Dkt Mwigulu amesema jitihada za kujenga viwanda haziwezi kuleta matokeo yaliyokusudiwa iwapo bidhaa zinazozalishwa hazitapata soko, hali inayoweza kupunguza uzalishaji, ajira na mapato ya Taifa.
Aidha, ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia sheria na kuzifanyia marekebisho pale inapobainika kuwa na mianya inayokwamisha matumizi ya bidhaa za ndani au kuruhusu kukwepa maelekezo ya Serikali.
Katika hatua nyingine, amewataka watendaji wa Serikali kuitambua sekta binafsi kama mshirika muhimu katika kujenga uchumi unaojitegemea, kwa kuheshimu mitaji na uwekezaji pamoja na kuweka mazingira rafiki ya biashara.
Kuhusu utekelezaji wa sera hizo, Waziri Mkuu ameielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara kuandaa mikakati madhubuti, kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wake, sambamba na kushirikiana na wizara nyingine na sekta binafsi.
Pia, ameitaka wizara kusimamia minyororo ya thamani ili kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kuzalisha malighafi na kutoa huduma zinazohitajika viwandani.
Amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na miundombinu ya nishati, maji, barabara na reli ili kuongeza ushindani wa viwanda vya Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema wizara imeandaa mkakati wa miaka 10 wa kutekeleza sera hizo, ukiwa na malengo ya kila mwaka yatakayofuatiliwa na kutathminiwa.
Amesema utekelezaji wake unalenga kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati pamoja na kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini, hususan katika ukanda wa Afrika.
Kapinga amesema kufikiwa kwa uchumi wa dola trilioni moja kunategemea mageuzi katika sekta ya viwanda yatakayochochea ukuaji wa uchumi.
Ameongeza kuwa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona sekta ya viwanda inakua na kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.
Katika hafla hiyo, Wizara ya Viwanda na Biashara ilitoa tuzo kwa Rais Samia kwa mchango wake katika kuwezesha mageuzi ya sekta ya viwanda, pamoja na kumtunuku Waziri Mkuu kwa kushiriki katika uzinduzi wa sera hizo.



