Kilimo chachangia mapato ya serikali Kigoma

KIGOMA; Mpango wa serikali mkoani Kigoma kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kubadili shughuli za kilimo kuwa biashara kimeifanya sekta hiyo kuchangia kuongeza mapato ya serikali sambamba na kuvutia watu wengi kujiingiza kwenye shughuli za kilimo kama ajira rasmi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Msaidizi Huduma za Uchumi na Uzalishaji katika Sekretariet ya Mkoa Kigoma, James Peter, wakati Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Serikali ya Korea (KOICA), Kim Sik Hyun alipofanya ziara na kutembelea mradi wa Kilimo Tija Kigoma (KITIKI) ambao unafadhiliwa na shirika hilo kwa ushirikiano na Shirika la Chakula la Umoja la Mataifa (WFP).

Peter alisema katika kipindi cha miaka mitatu, kilimo kimeongeza mapato ya serikali kwa asilimia 44 huku sekta hiyo ikikua kwa asilimia 17 na kusababisha kuongezeka kwa uzalishaji na matumizi ya pembejeo ikiwemo mbolea na mbegu bora kwa wakulima kwa asilimia 11.3.

Amesema hali hiyo imekifanya kilimo kuwa moja ya sekta za kimkakati katika masuala ya uchumi na biashara mkoani Kigoma kutoka kwenye kilimo cha kujikimu na kuwa biashara.
Akizungumzia kufanyika kwa mradi huo Sik Hyum alisema umekuwa kichocheo kikubwa katika kuboresha kilimo mkoani Kigoma na kuimarisha uchumi wa wakulima wa dogo, ili kukua na kukifanya kilimo kuwa shughuli kuu ya kiuchumi mkoani humo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa, Ronald Tran Ba Huy alisema kuwa kabla ya kuanzishwa kwa mradi wa KITIKI, shirika hilo lilikuwa likiagiza chakula mikoa mbalimbali kwa ajili ya wakimbizi mkoani Kigoma, lakini kwa sasa baada ya kuanza mradi huo na wakulima kujengewa uwezo shirika hilo linanunua sehemu kubwa ya mahindi na maharage kwa wakulima wa Kigoma.



