Watakiwa kujitokeza kujadili miradi ya maendeleo

MBEYA; Wafanyabiashara na wawekezaji jijini Mbeya wametakiwa kujitokeza katika vikao vya majadiliano ya miradi ya maendeleo wanapoalikwa na serikali ili kupata taarifa za fursa za uwekezaji na kujiandaa kushiriki katika utekelezaji wake,badala ya kusubiri miradi itangazwe ndipo waanze kuzitafuta fursa hizo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Jiji la Mbeya, Festo Nashon, wakati wa kikao cha majadiliano na wawekezaji pamoja na taasisi za kifedha kuhusu taarifa za upembuzi wa awali wa mradi wa ujenzi wa stendi mpya ya Uyole, unaotarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.
Nashon amesema ushiriki wa wawekezaji wazawa una umuhimu mkubwa kwa sababu wanafahamu mazingira ya biashara na uwekezaji katika maeneo yao hivyo wana nafasi nzuri ya kutambua fursa na changamoto zilizopo katika maeneo wanayokusudia kuwekeza.
Mkuu wa Idara ya Maandalizi na Uendelezaji wa Miradi kutoka Kituo cha Ubia (PPP) Innocent Mauki, amesema taasisi hiyo inaendelea kufanya ziara katika halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya kujadiliana na wadau kuhusu miradi inayotarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano na sekta binafsi.

“Ziara hii imelenga kupata maoni ya wawekezaji na wadau kuhusu mambo yanayopaswa kuzingatiwa na kuboreshwa katika maandiko ya miradi hiyo ili yaendane na mazingira ya uwekezaji pamoja na mahitaji halisi ya wananchi wa Mbeya,”amesema Mauki
Amesema Halmashauri ya Jiji la Mbeya ina miradi miwili inayotarajiwa kutekelezwa kwa mfumo wa ubia na sekta binafsi ukiwemo wa ujenzi wa Stendi mpya ya Uyole huku akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha miradi hiyo inakuwa na tija kwa wananchi , huku ikiwezekana pia kupata ufadhili au mikopo kutoka taasisi za kifedha.
Amesema ushiriki wa sekta binafsi katika miradi ya maendeleo ni nguzo muhimu ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, inayolenga kuifanya sekta binafsi kuwa mshiriki mkuu katika kukuza uchumi wa Tanzania kwa asilimia 70.
Mwakilishi wa wawekezaji, Mkuu wa Masoko wa Kampuni ya Maranatha, Shitindi Venance, amewahimiza Watanzania kutumia fursa zilizopo katika kipindi hiki akisema fursa hizo zinaweza kupungua kadiri muda unavyokwenda huku akiwahimiza vijana kuchangamkia fursa ya kubuni mifumo ya kidigitali katika itakayosaidia uendeshaji miradi hiyo.



