Bil 2/- kuwawezesha vijana, wanawake Kahama

KAHAMA: MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amekabidhi mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 2.167 kwa vikundi 96 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika Manispaa ya Kahama, akivitaka vikundi hivyo kuitumia fedha hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kukuza shughuli za kiuchumi na kujikwamua kimaisha.
Fedha hizo zilizotokana na mapato ya ndani ya Manispaa ni sehemu ya asilimia 10 inayotengwa kwa ajili ya kuwawezesha makundi hayo kiuchumi.
Akizungumza jana wakati wa hafla ya kukabidhi mikopo hiyo, Mhita alisisitiza umuhimu wa vijana waliopata mikopo hiyo kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha kwa kuzielekeza katika shughuli za uzalishaji badala ya kuzitumia katika anasa.
Alisema mikopo hiyo inapaswa kuwa chachu ya kukuza biashara, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wanufaika, huku akiwataka viongozi wa vikundi kuhakikisha fedha zinatumika kwa uaminifu na uwajibikaji.
“Kumbukeni fedha hizi ni mikopo inayopaswa kurejeshwa kwa wakati ili kutoa fursa kwa vikundi vingine kunufaika na mpango huo, unaolenga kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata mitaji,” alisema Mhita.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, alisema tangu kuanza kwa mpango huo mwaka 2025, halmashauri hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilionu 6.377 kwa vikundi 335 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Alisema katika robo ya kwanza na ya pili ya mwaka wa fedha 2026/2027, Manispaa imetoa Sh bilioni 2.167 kwa vikundi 96, ambapo vikundi 45 vya vijana vimepata Sh1.428 bilioni, vikundi 46 vya wanawake Sh708.52 milioni na vikundi vitano vya watu wenye ulemavu Sh31 milioni.
Kibetu alisema mikopo hiyo imewezesha wanufaika kununua maguta ya mizigo, bajaji na pikipiki za kusafirishia abiria, cherehani, kukuza mitaji ya biashara na kununua gari la kusafirisha samaki kutoka ziwani kwenda sokoni.
Alisema hatua hiyo imeongeza uwezo wa wanufaika kuendesha shughuli zao za kiuchumi na kupata kipato cha kujikimu kimaisha.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kahama, Kaniki Mataluma, alisema mikopo hiyo inayotokana na mapato ya ndani inalenga kuwawezesha makundi hayo kujitegemea kiuchumi na kupunguza utegemezi wa kifamilia.
Aliongeza kuwa katika mwaka ujao wa fedha, Manispaa inatarajia kutoa mikopo inayozidi Sh4 bilioni kwa ajili ya kuendeleza uwezeshaji wa makundi hayo.



