TPC yaeleza umuhimu wa ofisi za usimamizi miradi

MOROGORO:Shirika la Posta Tanzania (TPC) limeeleza umuhimu wa taasisi za umma kuwa na ofisi maalumu za usimamizi wa miradi, likisema mifumo hiyo inaweza kusaidia kuongeza ufanisi, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa katika Mkutano wa Mwaka wa Taasisi ya Wataalamu wa Usimamizi wa Miradi Tanzania (PMI Tanzania Project Management Week & Annual Conference 2026), uliofanyika Novemba 5, 2026, katika Cate Hotel, Morogoro.
Katika mjadala wa jopo kuhusu nafasi ya Ofisi za Usimamizi wa Miradi katika sekta ya umma, Meneja wa Ofisi ya Miradi wa Shirika la Posta Tanzania, Seleman Daffy, alishiriki kueleza uzoefu wa taasisi hiyo katika kutumia mfumo huo.
Daffy amesema mjadala huo ulitoa fursa kwa taasisi mbalimbali kubadilishana uzoefu na kujifunza namna ya kuimarisha mifumo ya usimamizi wa miradi, akibainisha kuwa uzoefu wa Posta unaweza kuwa rejea kwa taasisi nyingine zinazolenga kuboresha utekelezaji wa miradi yake.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi na Makamu wa Rais wa Masuala ya Wanaojitolea wa PMI Tanzania, Rahma Kova, amesema Posta ilipewa nafasi ya kushiriki kutokana na kuwa miongoni mwa taasisi chache nchini zilizoanzisha ofisi maalumu ya usimamizi wa miradi.
Mkutano huo uliwakutanisha wataalamu wa usimamizi wa miradi, viongozi wa taasisi na wadau mbalimbali kujadili mbinu za kuboresha usimamizi na utekelezaji wa miradi.
Ushiriki wa Posta katika mjadala huo unaibua mjadala mpana kuhusu umuhimu wa taasisi za umma kuwa na mifumo inayohakikisha miradi haisimamiwi kwa kuzingatia ukamilishaji pekee, bali pia matokeo, thamani ya rasilimali zilizotumika na manufaa kwa wananchi.



