Ndejembi atoa maagizo utekelezaji mradi wa umeme Kusini

RUVUMA: Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, ameitaka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuongeza usimamizi kwa Kampuni ya Kalpataru inayotekeleza mradi wa kusafirisha umeme wa kilovolti 220 kutoka Songea–Tunduru–Masasi, akieleza kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wake.

Amesema kasi ndogo ya kazi inachelewesha dhamira ya Serikali ya kuunganisha mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara na Gridi ya Taifa ili kuwawezesha wananchi kupata umeme wa uhakika.

Akizungumza Novemba 11, 2026, Ndejembi amesema mradi huo una umuhimu mkubwa katika kuimarisha usafirishaji wa umeme na kufungua fursa za kiuchumi katika sekta za madini, kilimo na uzalishaji viwandani.

Amesema Wilaya ya Tunduru imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya umeme wa uhakika kutokana na kutegemea umeme unaosafirishwa kutoka umbali mrefu, huku mahitaji yake ya juu yakifikia megawati nne.

“Mradi huu ni muhimu kwa kuwa utachangia Mikoa ya Kusini kuunganishwa na Gridi ya Taifa. Mahitaji ya juu ya wananchi wa Tunduru ni megawati nne, ambazo zinasafiri umbali mrefu, hivyo kusababisha changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika,” amesema.

Amesema Serikali imetoa zaidi ya Sh bilioni 42 kwa ajili ya kuharakisha utekelezaji wa mradi huo, kama ilivyoombwa na mkandarasi, lakini kasi ya kazi bado haiendani na makubaliano yaliyofikiwa.

Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema sehemu ya mradi kutoka Tunduru hadi Masasi ilikuwa imefikia asilimia sita kabla ya Serikali kutoa fedha, lakini sasa imeongezeka hadi asilimia 35, huku sehemu ya Songea–Tunduru ikifikia asilimia 58.

Amesema Wizara itahakikisha mkandarasi anasimamiwa ipasavyo ili mradi ukamilike ifikapo Septemba 30, 2027.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema sehemu ya Songea–Tunduru yenye urefu wa kilomita 214.5 inatekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 151, huku sehemu ya Tunduru–Masasi yenye urefu wa kilomita 177 ikigharimu Sh bilioni 158.

Amesema mradi huo ni sehemu ya miradi 27 ya Gridi Imara inayotekelezwa na Serikali kupitia TANESCO kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini.

Katika Kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Tunduru, amesema kutafungwa transfoma mbili zenye uwezo wa MVA 60 kila moja, pamoja na matoleo 10 ya msongo wa kilovolti 33 yatakayohudumia maeneo mbalimbali.

Mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya Kalpataru ya India unatarajiwa kukamilika Septemba 30, 2027, ukiwa na matarajio ya kuimarisha huduma ya umeme na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Mikoa ya Kusini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button