Mkurugenzi ataja mbinu kuongeza uelewa kwa wanafunzi

DAR ES SALAAM: MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Uwezo Tanzania, Baraka Mgohamwende amesema matumizi ya michezo katika ufundishaji yanaweza kuwa suluhisho la kupunguza adhabu ya viboko shuleni na kuongeza uelewa wa wanafunzi.

Mgohamwende alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumzia Tathmini ya Ujifunzaji ya mwaka 2026 inayotekelezwa na shirika hilo katika mikoa yote 31 ya Tanzania pamoja na Unguja na Pemba.

Alisema ni muhimu kwa walimu kutumia mbinu zinazowashirikisha wanafunzi katika mchakato wa kujifunza, badala ya kutegemea viboko kama njia ya kuwafanya watoto waelewe masomo.

“Mbinu ya ufundishaji ya Darasa Jifunze inayomshirikisha mwanafunzi kupitia michezo inasaidia kujenga mazingira rafiki ya kujifunzia na kumwezesha mtoto kuelewa masomo kwa vitendo badala ya kutegemea adhabu,’’alisema Mgohamwende.

Alieleza kuwa mazingira bora ya ujifunzaji yanapaswa kumwezesha mtoto kushiriki, kuuliza maswali na kujenga uelewa bila hofu ya kuadhibiwa.

Awali alieleza kuwa Uwezo Tanzania inakaribia kukamilisha ukusanyaji wa takwimu za tathmini hiyo inayolenga kubaini hali halisi ya ujifunzaji kwa watoto wenye umri wa miaka mitano hadi 17.

Alisema tathmini hiyo imehusisha kaya 23,052 katika maeneo 1,151 ya kuhesabia watu, ikitekelezwa kwa ushirikiano na wawezeshaji wa jamii takribani 1,100 pamoja na washirika 14 wa utekelezaji.

Mgohamwende alisema kuwa kuwa mtoto amesajiliwa shuleni hakumaanishi moja kwa moja kwamba anapata maarifa yanayotarajiwa.

Alisema ni muhimu kupima kile ambacho watoto wanaweza kufanya ili kubaini mapungufu yaliyopo na kuweka mikakati ya kuboresha matokeo ya ujifunzaji.

‘’Tathmini hiyo inapima stadi za kusoma na kuandika, kuhesabu, stadi za maisha pamoja na maadili, ikiwa ni upanuzi wa tathmini za awali ambazo zilijikita zaidi katika kusoma na kuhesabu,’’alisema.

Alisema kwa upande wa stadi za maisha, tathmini inalenga kubaini uwezo wa watoto kukabiliana na changamoto za kila siku, wakati kipengele cha maadili kikihusisha misingi kama heshima, uwajibikaji na mahusiano mazuri katika jamii.

Pia alisema matokeo ya tathmini hiyo yanatarajiwa kutumika katika mijadala ya kisera na kuboresha mipango ya elimu, mbinu za ufundishaji na ugawaji wa rasilimali ili kuhakikisha watoto wanapata stadi zinazohitajika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button