JK asisitiza uwekezaji wa mafunzo kuimarisha tiba ya dharura

Arusha : Rais Mstaafu Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amesema uwekezaji katika mafunzo na uendelezaji wa wataalamu wa afya ndio msingi muhimu wa kuimarisha huduma za tiba ya dharura nchini na kuokoa maisha ya wagonjwa.
Dk. Kikwete amesema uwepo wa majengo na vifaa tiba vya kisasa pekee hauwezi kuleta matokeo yanayotarajiwa bila kuwa na wataalamu wenye ujuzi, maarifa na dhamira ya kutoa huduma bora.
Akizungumza kama mgeni maalumu katika Mkutano wa Nane wa Afrika wa Tiba ya Dharura (AfCEM 2026), unaofanyika jijini Arusha, Dk. Kikwete amesema uamuzi wa kuanzisha idara ya kwanza ya tiba ya dharura katika Hospitali ya Taifa Muhimbili mwaka 2010 ulienda sambamba na mkakati wa kuanzisha mafunzo rasmi katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
–

Amesema lengo lilikuwa kujenga mfumo endelevu wa kuzalisha madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa fani hiyo.
Amesema safari ya kuimarisha huduma za tiba ya dharura nchini ilianza mwaka 2007 alipokutana na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Abbott Fund, ambapo walijadili namna ya kuboresha huduma za maabara katika hospitali za mikoa 23 pamoja na changamoto ya vifo vya wagonjwa mahututi na majeruhi vilivyotokana na kukosekana kwa mfumo madhubuti wa kuwahudumia wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka.

Ameeleza kuwa wakati huo, wagonjwa waliofika hospitalini walipokelewa katika sehemu za mapokezi, kupimwa viashiria vya afya na kuamuliwa kama walazwe au waendelee na matibabu ya kawaida, bila kuwepo mfumo imara wa kuwatambua mapema na kuwapa kipaumbele wagonjwa waliokuwa katika hali zinazohatarisha maisha.



