RAAWU waonywa rushwa kwenye uchaguzi

MBEYA; Katibu Mkuu wa Chama Cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu,Sayansi, Teknolojia, Utafiti na Habari (RAAWU), Joseph Sayo amewaonya wanachama wa chama hicho kuepuka vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi wa viongozi , akisisitiza kuwa kiongozi anayepatikana kwa njia ya rushwa ni vigumu kumwajibisha.
Sayo ametoa onyo hilo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Saba wa RAAWU,Kanda ya Nyanda za Juu Kusini uliofanyika jijini Mbeya.
“Ukipokea rushwa umeuza haki yako,na huyo kiongozi aliyechaguliwa huwezi kuwa na nguvu ya kumkemea,”amesema Sayo.

Aidha amewataka wanachama kuchagua viongozi kulingana na utendaji kazi na uadilifu,na uwezo wa kuwatumikia wanachama, akisisitiza viongozi watakaochaguliwa kuwasimamia ipasavyo maslahi ya wanachama na kutetea haki zao.
Amewataka wanachama kutokukubali kugawanywa na misimamo ya wachache inayolenga kukibomoa chama hicho ,huku akionya wagombea watakaoshindwa katika uchaguzi kuacha kushawishi wanachama kujiondoa katika Chama hicho.
Mkutano huo umefanyika sambamba na uchaguzi wa viongozi mbalimbali wa Kanda hiyo,ambapo kwa upande wa nafasi ya Mwenyekiti wa Kanda,S adick Msilwa kutoka VETA-Mbeya ameibuka mshindi.



