Ripoti yaanika chanzo mgogoro Wamachinga, bajaji Mbeya

MBEYA; Timu iliyoundwa na Serikali kutathmini changamoto zilizosababisha mgogoro kati ya mamlaka za Serikali, waendesha bajaji na machinga jijini Mbeya, imewasilisha ripoti yake na kubainisha sababu mbalimbali zilizosababisha baadhi ya wahusika kukaidi agizo la kuhamia maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli zao.

Katika taarifa hiyo, timu imebaini kuwa ukaidi huo haukutokana na bahati mbaya, bali ulichangiwa na changamoto za kuingiliwa kwa masuala ya kisiasa,miundombinu isiyokidhi mahitaji, udhaifu wa usimamizi wa taasisi husika, pamoja na ushirikishwaji hafifu wa wadau katika maamuzi.

Awali,Oktoba 12, Serikali ya Mkoa wa Mbeya ilitoa tamko lililowataka machinga na waendesha bajaji kuondoka katika maeneo yasiyo rasmi na kuhamia maeneo yaliyotengwa na Serikali kwa lengo la kupunguza msongamano, migogoro na uvunjifu wa sheria katika Jiji la Mbeya na Mji wa Mbalizi.

Katika tamko hilo, wahusika walipewa notisi ya siku saba, hata hivyo baadhi yao walikaidi agizo hilo na kuendelea na shughuli zao katika maeneo yasiyoruhusiwa, hali iliyosababisha mvutano kati yao na mamlaka za usimamizi na kuvuruga utulivu wa shughuli za biashara na usafiri.

Hatua hiyo ilimlazimu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, kufanya ziara mkoani humo Oktoba 22, na kumuelekeza mkuu wa mkoa huo,kuunda timu maalumu ya kutathmini hali hiyo na kuandaa mapendekezo ya namna bora ya kutatua changamoto zilizojitokeza.

Akiwasilisha taarifa ya timu hiyo, Mwenyekiti wa timu hiyo Notker Kilewa, amesema ili kukabiliana na changamoto hizo, timu imependekeza bajaji kugawanywa katika makundi nane na kutambulishwa kwa mikanda ya rangi, kusitishwa kwa muda usajili wa bajaji mpya pamoja na bajaji kutumia barabara za pembezoni mwa mji, daladala kutumia barabara kuu.

Amesema tume imeshauri pia siasa zisitumike katika utatuzi wa changamoto tajwa badala yake kuwepo kwa mfumo shirikishi unaowahusisha wadau wote huku ikipendekeza pia kuboreshwa kwa miundombinu ya masoko, kufunguliwa kwa vyumba vya biashara vilivyofungwa na masoko rasmi kuunganishwa na vituo vya usafiri.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Jumanne Sagini ameagiza watendaji wanaohusika na changamoto zilizotajwa kuzitatua huku akiagiza pia vyombo vya usalama kuchukua hatua kwa wote watakaokaidi maazimio yaliyokubaliwa na wadau, kwa kuwa pande zote zimeshirikishwa katika mchakato huo.

Amesema utekelezaji wa mpango huo utaanza Novemba 15 mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha Jiji la Mbeya linakuwa na mpangilio bora wa usafiri na biashara.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button