Bukoba yatakiwa kuharakisha miradi ya maendeleo

BUKOBA: MKUU wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akieleza kutoridhishwa na kasi ya baadhi ya miradi licha ya fedha na wakandarasi kuwepo.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Bukoba, Sima ameitaka Halmashauri kupitia kwa Mkurugenzi na wakuu wa idara kuimarisha usimamizi wa miradi, ikiwemo inayotekelezwa kupitia Mpango wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC), ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Amesisitiza umuhimu wa kusimamia kwa karibu ujenzi wa soko, barabara na mradi wa kingo za Mto Kanoni, akieleza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutarahisisha shughuli za wafanyabiashara, kuboresha mazingira ya biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.

Aidha, ameitaka Halmashauri kuimarisha usimamizi wa ofisi za kata na mitaa, utatuzi wa migogoro ya ardhi na upangaji wa mji, huku akiwaonya viongozi wa mitaa wanaotumia vibaya madaraka yao katika masuala ya uuzaji wa maeneo.

Katika suala la usafi wa mazingira, Sima amesisitiza ushirikiano kati ya Halmashauri, kampuni za ukusanyaji taka na viongozi wa mitaa ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi katika maeneo yote kwa kuzingatia mipango ya kila kata.

Pia, ameitaka Halmashauri kuimarisha usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, akisisitiza umuhimu wa kuhakiki waombaji kwa kushirikisha madiwani na watendaji wa maeneo husika.

Kuhusu huduma ya maji, ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) kupitia upya utaratibu wa uwekaji wa mita ili kuondoa malalamiko ya wananchi wanaotozwa gharama za ziada za kuhamisha au kurejesha mita za maji.

Vilevile, amewataka wazazi, walezi na viongozi wa maeneo kuongeza uangalizi kwa watoto wa kike kutokana na mwenendo wa baadhi ya wasichana wadogo kukutwa katika maeneo yasiyo salama nyakati za usiku, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kulinda usalama wao.

Kwa upande wao, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Mhandisi Johnston Mtasingwa, na Meya wa Manispaa hiyo, Acton Rankomez, wameahidi kushirikiana na Halmashauri kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ili kuimarisha utekelezaji wa miradi na huduma za maendeleo kwa wananchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button