Tanzania yalenga kuvutia mitaji nishati safi ya kupikia

UTURUKI: TANZANIA imepanua juhudi za kutafuta uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya nishati, ikilenga kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Jitihada hizo zimejadiliwa katika Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), unaoendelea jijini Antalya, Uturuki, ambako Waziri wa Nishati, Dk Juma Homera, ameshiriki mijadala ya ngazi ya juu kuhusu mpito wa nishati safi, usalama wa nishati na upatikanaji wa umeme.
Katika mjadala uliofanyika Novemba 11, 2026, kuhusu mpango wa kimataifa wa kuongeza mchango wa umeme katika matumizi ya nishati duniani kufikia asilimia 35 ifikapo mwaka 2035, Homera, aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania inaunga mkono mpango huo na inaendelea kuimarisha sekta ya umeme.

Amesema uwezo wa uzalishaji umeme nchini umefikia zaidi ya megawati 4,600, huku vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vikiwa vimefikiwa na miundombinu ya umeme.
Ameeleza kuwa kupitia Mpango wa Taifa wa Nishati, Serikali inalenga kuongeza kiwango cha uunganishaji wa umeme kufikia asilimia 75 ifikapo mwaka 2030, sambamba na kuongeza mchango wa nishati jadidifu katika uwezo wa uzalishaji umeme kufikia asilimia hiyo.
Katika hatua nyingine, Homera ameshiriki mjadala kuhusu umuhimu wa miundombinu ya gridi za umeme katika kuimarisha usalama wa nishati na maendeleo ya kiuchumi kupitia Mpango wa Kimataifa wa Kuharakisha Maendeleo ya Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (Global Grid Accelerator).
Katika mikutano ya uwili, Waziri huyo amekutana na Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Nishati Endelevu kwa Wote, ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Shirika la Sustainable Energy for All (SEforALL), Damilola Ogunbiyi, ambapo wamejadiliana namna ya kuimarisha ushirikiano katika kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mazungumzo hayo yamejikita katika kupanua matumizi ya nishati safi katika taasisi za umma, hususan shule na vituo vya afya, pamoja na kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya uwekezaji katika eneo hilo.

Ogunbiyi ameipongeza Tanzania kwa juhudi zake za kuendeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia barani Afrika na kueleza utayari wa SEforALL kuendelea kushirikiana na Serikali kuharakisha utekelezaji wa mipango hiyo.
Aidha, Homera amekutana na uongozi wa kampuni ya UpEnergy kujadili fursa za kutumia mifumo ya biashara ya hewa ukaa (Carbon Credits) kuvutia uwekezaji na kupunguza gharama za teknolojia za nishati safi ya kupikia.
Amesema biashara ya hewa ukaa inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuvutia uwekezaji na kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi na taasisi mbalimbali.
Ushiriki wa Tanzania katika mikutano hiyo unaendana na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.



