Serikali yataka taasisi kuwekeza kwenye teknolojia

ARUSHA; SERIKALI imetaka taasisi za umma na binafsi kuwekeza katika teknolojia za kisasa zitakazowezesha kubaini viashiria vya udanganyifu wa kidijitali mapema na kuzuia vitendo hivyo kabla havijasababisha hasara.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray, leo jijini Arusha, wakati akifungua Kongamano la Mwaka la Chama cha Wachunguzi wa Udanganyifu Tanzania (ACFE Tanzania), lililojadili namna ya kukabiliana na udanganyifu katika zama za akili mnemba (AI), takwimu kubwa na fedha za kidijitali.
Regina amesema maendeleo ya teknolojia yameleta fursa za kuboresha utoaji wa huduma, uwazi na ufanisi katika taasisi, lakini pia yameibua vihatarishi vipya vya udanganyifu, ikiwemo matumizi ya akili mnamba kutengeneza utambulisho bandia, kughushi sauti na picha, pamoja na kufanya miamala isiyo halali.
Amesema hali hiyo inahitaji taasisi kuachana na utegemezi wa mifumo ya zamani ya udhibiti na kuwekeza katika mifumo ya kisasa inayoweza kutambua viashiria vya udanganyifu kwa wakati na kuchukua hatua za haraka kabla madhara hayajatokea.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha uwazi, uwajibikaji na uadilifu kupitia Mkakati wa Taifa wa Kupambana na Rushwa na Mpango wa Utekelezaji Awamu ya Nne (NACSAP IV), huku akisisitiza kuwa kila mtumishi wa umma ana wajibu wa kulinda rasilimali za Taifa na kuzuia matumizi mabaya ya mamlaka na fedha za umma.
Kwa upande wake, Rais wa ACFE Tanzania, Ali Mabrouk Juma, amesema chama hicho kinalenga kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani katika kuzuia, kubaini na kuchunguza udanganyifu kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, huku kikishirikiana na taasisi nyingine bila kuingilia mamlaka yao ya kisheria.
Amesema ACFE Tanzania pia inashiriki katika maandalizi ya Mpango Mkakati wa Taifa wa Kuzuia Udanganyifu na kupendekeza kutambuliwa na kuendelezwa kwa kada ya wachunguzi wa udanganyifu katika sekta ya umma na binafsi, ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na vitendo hivyo.
Naye Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Wizara ya Fedha, Mhandisi Kenneth Nindie, amesema Serikali imechukua hatua za kuimarisha usimamizi wa vihatarishi vya udanganyifu, ikiwemo kutoa Mwongozo wa Usimamizi wa Vihatarishi vya Udanganyifu katika Taasisi za Umma mwaka 2023 na kuandaa Mfumo wa Kielektroniki wa Taarifa za Usimamizi wa Vihatarishi katika Taasisi za Serikali (GERMIS), utakaosaidia taasisi kutambua na kufuatilia vihatarishi kwa wakati halisi.



