Boom yamwingizia Rehema Sh milioni 2.6

IRINGA: MWANAFUNZI wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Iringa, Rehema Haji Soza, amenufaika kwa kupata zaidi ya Sh milioni 2.6 baada ya kueleza namna anavyotumia sehemu ya fedha za kujikimu chuoni, maarufu kama boom, kununua hisa katika taasisi za kifedha.
Rehema, anayesomea Shahada ya Sayansi ya Uhasibu na Fedha, alipata fursa hiyo baada ya kushiriki kongamano la Campus Connect lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Mkwawa, mkoani Iringa, ambako alishinda shindano la Bonga na Waziri.
Akizungumza katika kongamano hilo, Rehema alisema kati ya Sh600,000 anazopokea kama fedha za kujikimu, amekuwa akitenga Sh200,000 kwa ajili ya kununua hisa katika Benki za CRDB, NMB na taasisi zingine za kifedha.
Alisema alianza utaratibu huo kwa kuona umuhimu wa kutumia sehemu ya fedha anazopata chuoni kuwekeza, badala ya kuzitumia zote kwa mahitaji ya kila siku.
“Nilipokuwa napata boom, nilikuwa natenga Sh200,000 na kununua hisa katika taasisi hizo za kifedha,” alisema.

Ufafanuzi wake kuhusu uwekezaji wa hisa ulivutia washiriki wa kongamano hilo, baada ya kuulizwa swali kuhusu anachokifahamu katika eneo hilo na hatimaye kuingizwa kwenye shindano la Bonga na Waziri.
Katika shindano hilo lililokuwa na washiriki watano, waliopimwa kwa vigezo vya ujasiri, uelewa na ushiriki, Rehema alishika nafasi ya kwanza, huku Jesca akipata nafasi ya pili na kujinyakulia Sh 400,000.
Kutokana na ushindi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Dk Joel Arthur Nanauka, aliahidi kumwongezea hisa zenye thamani ya Sh500,000 katika Benki ya CRDB.
Benki ya CRDB nayo iliahidi kuongeza hisa za Sh500,000, huku mwakilishi wa Soko la Hisa akitoa Sh500,000 na Msaidizi wa Naibu Katibu Mkuu naye akiahidi kiasi kama hicho.
Michango na ahadi hizo zilifikia Sh milioni mbili, huku zawadi nyingine alizopata kutokana na ushindi wake zikifanya jumla ya fedha na ahadi alizopata kuwa Sh milioni 2.6.
Aidha, Serikali iliahidi kumshirikisha Rehema katika majukwaa mengine kama hayo ili kutoa uzoefu wake na kuhamasisha vijana kutumia sehemu ya fedha wanazopata kuwekeza na kujenga uchumi wao.
Katika hatua nyingine, kongamano hilo lilikuwa na shindano la Idea Challenge lililolenga kutambua na kukuza ubunifu wa vijana katika biashara na ujasiriamali.

Katika shindano hilo, Ntihindu Esdras, mwenye kiwanda cha kutengeneza viatu vya wanafunzi, alishika nafasi ya kwanza na kujinyakulia Sh milioni tatu.
Baraka Wilbroad, anayejihusisha na uzalishaji wa maziwa ya soya, alishika nafasi ya pili na kunyakua Sh Milioni mbili, huku Enesta Mayeota, mwenye kiwanda cha kutengeneza nguo za wanawake, akishika nafasi ya tatu na kupata Sh Milioni 1.5, zote zikitolewa kwa udhamini wa benki ya CRDB.
Akizungumza katika kongamano hilo, Dk Nanauka aliwataka vijana kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kujiajiri, kuanzisha biashara na kushiriki katika shughuli za maendeleo badala ya kusubiri kuajiriwa.
Alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira ya kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi, ikiwemo utaratibu wa kutenga asilimia 30 ya manunuzi ya umma kwa makundi maalumu, yakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Alitaja huduma zinazoweza kutolewa na kampuni za vijana kupitia fursa hizo kuwa ni usafi wa ofisi za Serikali, usambazaji wa vifaa vya maandishi, huduma za chakula na vinywaji, utangazaji na utengenezaji wa nembo za taasisi.
Aliwataka pia wanafunzi kutumia muda wao vyuoni kujenga maarifa, ubunifu na mahusiano ya kimkakati yatakayowawezesha kutambua na kutumia fursa zilizopo katika jamii.
l



