Bodaboda kuwa walinzi haki za walaji

DODOMA: WAKALA wa Vipimo Mkoa wa Dodoma umewataka maafisa usafirishaji, wakiwemo waendesha bodaboda, kuhakikisha bidhaa wanazonunua kwa niaba ya wateja zinapimwa kwa usahihi ili kulinda haki za walaji na kudhibiti udanganyifu wa vipimo.

Wakala huo umesema maafisa hao wana nafasi muhimu katika kulinda maslahi ya wananchi kutokana na jukumu lao la kuunganisha wafanyabiashara na wateja, hususan katika ununuzi wa bidhaa zinazohitajika majumbani.

Akizungumza wakati wa kutoa elimu hiyo jana jijini Dodoma, Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Dodoma, Edward Patrick, alisema baadhi ya maafisa usafirishaji hawana utaratibu wa kuthibitisha uzito au kiasi cha bidhaa wanazonunua kabla ya kuzichukua na kuwalipia wateja.

Alisema hali hiyo inaweza kusababisha malalamiko ya upungufu wa bidhaa na migongano kati ya wateja na madereva, ambao wakati mwingine hujikuta wakilaumiwa kwa bidhaa walizowafikishia.

“Ni wajibu wa afisa usafirishaji anapoenda kununua gesi kuhakikisha inapimwa na kujiridhisha kuwa kiasi kilichopo ni sahihi kabla ya kulipa na kuondoka na mtungi,” alisema.

Patrick alisema changamoto hiyo pia inajitokeza katika ununuzi wa nyama, ambapo baadhi ya wateja huagiza kiasi maalumu kwa njia ya simu bila kushuhudia upimaji, hivyo madereva wanapaswa kuhakikisha wanakuwepo wakati bidhaa inapopimwa.

Alisisitiza umuhimu wa kutumia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo, yenye stika halali ya uhakiki na iliyo katika hali nzuri ya kufanya kazi.

Aidha, alisema bidhaa zinazouzwa kwa uzito, zikiwemo viazi na mazao mengine sokoni, zinapaswa kupimwa kwa mizani badala ya kutegemea makadirio ili kuhakikisha mnunuzi anapata kiasi anachostahili.

Alisema Wakala umeamua kuwashirikisha maafisa usafirishaji katika elimu hiyo kutokana na nafasi yao ya kuwafikia wananchi wengi, wakiwemo wale ambao hawapati fursa ya kushiriki mikutano ya elimu kwa walaji.

Alitaja hatua nyingine zinazochukuliwa na Wakala kuwa ni kutoa elimu kupitia klabu za vipimo shuleni na kuwashirikisha madiwani ili kusaidia kufikisha ujumbe kwa wananchi katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Huduma za Usafirishaji Mkoa wa Dodoma, Baraka Obadia Mbuhe, alisema elimu hiyo itawasaidia maafisa usafirishaji kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na kulinda imani ya wateja.

Alisema madereva wanapaswa kuhakikisha bidhaa wanazoagizwa kununua, zikiwemo gesi, nyama, vyakula na nafaka, zinapimwa kwa usahihi kabla ya kuzichukua na kuzikabidhi kwa wateja.

“Tunapoagizwa kununua gesi, tunapaswa kumtaka muuzaji aipime na kuhakikisha uzito wake unalingana na ulioandikwa kwenye mtungi. Hali kadhalika, tunaponunua nyama au nafaka, lazima tuhakikishe vimepimwa kwa mizani sahihi,” alisema.

Alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza migongano kati ya wateja na maafisa usafirishaji, ambao wanaweza kulaumiwa kwa upungufu wa bidhaa iwapo hawakushuhudia upimaji wake.

Alisisitiza pia umuhimu wa kukagua stika za Wakala wa Vipimo kwenye mizani na vifaa vingine vya kupimia, akisema elimu hiyo inapaswa kuwafikia maafisa usafirishaji katika mikoa yote nchini.

Naye Msemaji Mkuu wa Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dodoma, Simon Elias Mangula, aliushukuru Wakala wa Vipimo kwa kuwashirikisha madereva katika elimu hiyo, akisema wana nafasi muhimu ya kulinda haki za wananchi kutokana na ushiriki wao wa mara kwa mara katika manunuzi ya bidhaa mbalimbali.

Alisema ushirikiano huo ni muhimu katika kujenga jamii inayozingatia matumizi sahihi ya vipimo, huku akiwataka madereva kuwa waaminifu wanapotekeleza maagizo ya wateja na kuhakikisha bidhaa zinapimwa kwa usahihi.

“Elimu hii itaongeza uelewa wa walaji, kupunguza malalamiko na kuimarisha haki katika shughuli za manunuzi na biashara,” alisema.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button