Waomba kikosi maalumu kuchunguza mauaji ya wanawake

ARUSHA; Watetezi wa haki za wanawake na mitandao inayopinga ukatili wa kijinsia mkoani Arusha wameiomba Serikali kuunda kikosi maalumu ndani ya Jeshi la Polisi kitakachokuwa na jukumu la kufuatilia na kuchunguza matukio ya mauaji ya wanawake nchini.

Watetezi hao wamesema lengo la kikosi hicho ni kuhakikisha wahusika wa mauaji hayo wanabainishwa haraka na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Wametoa wito huo wakati wakizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, wakieleza wasiwasi wao kuhusu kuendelea kujitokeza kwa matukio ya mauaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake.Wamesisitiza kuwa ni muhimu vyombo vya dola kuimarisha mifumo ya ulinzi na usalama ili kukomesha vitendo hivyo.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CAIC Tanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa Dunia Salama Foundation, Idd Ninga, amekemea vikali matukio hayo.

Ninga ameiomba Serikali, kupitia vyombo vya dola, kuhakikisha wote wanaohusika na mauaji ya wanawake wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, akisisitiza kuwa hatua kali zinahitajika ili kuzuia vitendo hivyo kujirudia.

Amesema pamoja na kuunda kikosi maalumu cha Polisi, Serikali inapaswa kuanzisha kampeni za kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia na namna ya kuuzuia.

Pia amevitaka vyombo vya habari kutumia nafasi yake kuelimisha wananchi, kuibua matukio ya ukatili na kutoa taarifa zitakazosaidia kukabiliana na tatizo hilo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button