‘AI isiwe mbadala ujuzi wa watumishi’

MOROGORO: SERIKALI imewaelekeza watendaji wake kuhakikisha matumizi ya teknolojia ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI) yanapaswa kuzingatia uhakiki wa taarifa, usalama wa data, uadilifu na viwango vya kitaalamu.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu  Mkuu ,Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dk  Jim Yonazi, wakati akifungua mafunzo  ya siku tatu ya kimkakati ya uongozi katika Ufuatiliaji na Tathmini kwa ajili ya utawala unaotegemea Ushahidi , mjini Morogoro.

Mafunzo hayo yanawashirikisha Wakurugenzi wa Mipango na wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara pamoja na wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Sekretarieti za Mikoa huku yakilenga kuongeza uwezo wa viongozi na wataalamu katika Ufuatiliaji, Tathmini, Utafiti na Ujifunzaji (MERL).

Dk Yonazi amesema kuwa teknolojia ya  Akili Unde  inapaswa kuwa nyenzo ya kuongeza uwezo wa kitaalamu , kurahisisha  utendaji kazi, kuongeza ufanisi na kuboresha ubora wa huduma na  si mbadala wa utaalamu wa watumishi kuwaondolea  majukumu yao.

Amesema  Serikali inaendelea  kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mfumo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini kwa kuweka miundo ya kitaasisi, kuandaa miongozo na kujenga uwezo wa watumishi wake .

Dk Yonazi amesema mafanikio ya mfumo huo hayatapimwa kwa wingi wa taarifa zinazokusanywa, bali kwa namna ushahidi unaozalishwa unavyotumika kuboresha maamuzi na utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

“ Wataalamu hawapaswi kuishia kuandaa taarifa za utekelezaji kwa ajili ya kuripoti, bali wanapaswa kuwasaidia viongozi kubaini changamoto, kuelewa sababu za matokeo yaliyopatikana na kupendekeza hatua zinazofaa za kuboresha utendaji” amesema Dk Yonazi

Katibu Mkuu amesema kuwa taarifa zinazozalishwa zinapaswa kuwa sahihi, za kuaminika na kupatikana kwa wakati ili ziweze kusaidia viongozi kufanya maamuzi sahihi ya kisera na kiutendaji.

Dk Yonazi amewataka  watendaji kutumia TEHAMA na mifumo ya kisasa kuimarisha usimamizi, uchambuzi na uwasilishaji wa taarifa, na kuboresha mwingiliano wa mifumo ya Serikali ili kupunguza mlolongo  wa ukusanyaji wa taarifa.

Amesema mifumo ya Mipango na Ufuatiliaji na Tathmini katika taasisi za Serikali inapaswa kuendana na vipaumbele vya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ili kuwezesha kupima mchango wa kila taasisi katika kufikia malengo ya kitaifa, kubaini changamoto na kuweka hatua za ziada pale inapohitajika.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ufuatiliaji na tathimini ya utendaji wa serikali , kutoka katika ofisi hiyo ya  Waziri mkuu , Sakina Mwinyimkuu amesema  mafunzo hayo awamu inayofuata yatatolewa kwa  makatibu wakuu, manaibu makatibu wakuu, makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri nchini na waratibu wa mipango wa mikoa.

“Mafunzo haya yalikuwa yakifanyika kwa watumishi wa ngazi za chini kuanzia mwaka 2022 na sasa tumeamua kushirikisha viongozi wa ngazi za juu ili utekelezaji wake uwe rahisi ” amesema  Mwinyimkuu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button