Rais Samia awataka vijana kulinda amani

MOSHI: Rais Dk Samia Suluhu Hassan, amewataka vijana kulinda amani na usalama wa nchi wakati Tanzania ikijiandaa kupokea wageni wengi wa kimataifa watakaohudhuria shughuli na matukio mbalimbali nchini.

Rais Samia ametoa wito huo Novemba 20, alipokuwa akisalimia wananchi wa Bomang’ombe, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, akiwa njiani kuelekea mjini Moshi.

Amesema ongezeko la watalii wanaoingia nchini pamoja na mikutano ya kimataifa inayofanyika Tanzania ni kielelezo cha nchi kuendelea kuwa salama, hivyo amewataka wananchi kuendeleza hali hiyo.

“Ombi langu kwenu ni amani na utulivu kwa nchi yetu,” amesema Rais Samia.

Ametaja mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 pamoja na mashindano ya urembo wa dunia mwaka huo kuwa miongoni mwa matukio yanayotarajiwa kuleta wageni wengi nchini, hivyo kusisitiza umuhimu wa kulinda amani na utulivu.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Serikali imetenga tena fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko la kimataifa wilayani Hai, ambalo litawapa wakulima sehemu ya uhakika ya kuuza mazao yao.

“Ninataka niwahakikishie, tunakwenda kujenga soko la kimataifa ndani ya wilaya hii,” amesema.

Rais Samia yupo mjini Moshi kwa ajili ya kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maofisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi, unaofanyika katika Shule ya Polisi mjini humo.

 

Aidha, ameahidi kurejea mkoani Kilimanjaro kwa ziara rasmi ya kikazi, ambapo atatembelea miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi wa mkoa huo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button