Wawekezaji waalikwa sekta milki ya makazi

DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amezikaribisha kampuni na wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta ya milki ya makazi nchini, akieleza kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya uwekezaji katika ardhi.
Amesema ardhi ni rasilimali muhimu kiuchumi, ambayo mchango wake katika maendeleo unategemea namna inavyopimwa, kusajiliwa, kupangwa na kusimamiwa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akifungua Maonesho ya Jukwaa la Majadiliano ya Sekta ya Milki ya Makazi (Tanzania Real Estate Expo – TAREX 2026), yaliyoandaliwa na Imperial Marketing and Communications Limited katika ukumbi wa Super Dome, jijini Dar es Salaam.

Amesema makazi yaliyotawanyika yanasababisha Serikali kukabiliwa na gharama kubwa za kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi, ikiwemo umeme, maji, shule na barabara.
Ameeleza kuwa wakati mwingine Serikali inapokamilisha kusogeza huduma ya umeme katika eneo fulani, baada ya muda mfupi makazi mapya huanzishwa mbali na eneo hilo, hali inayolazimu kupanga upya gharama za kupeleka huduma hiyo. Amesema hali kama hiyo hutokea pia katika upatikanaji wa huduma nyingine za kijamii.
Amesema endapo makazi yatapangwa vizuri tangu mwanzo, Serikali itaweza kutumia rasilimali chache kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi.

Waziri Mkuu amesema Serikali haitaki maendeleo ya sekta ya milki yapimwe kwa wingi wa majengo yanayojengwa pekee, bali pia kwa mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kuboresha mazingira ya makazi na kuhakikisha wananchi wanamudu gharama za nyumba.
Amesisitiza umuhimu wa kuongeza upatikanaji wa nyumba zinazomudu gharama zake, hususan kwa vijana wanaohitimu vyuo vikuu na makundi mengine yanayokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa makazi.
Amesema takribani asilimia 70 ya wakazi wa mijini nchini wanaishi katika makazi yasiyo rasmi, hali inayohitaji ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kurasimisha maeneo, kuendeleza makazi yaliyopangwa na kuongeza upatikanaji wa nyumba bora zinazomudika.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya kifedha na kuandaa miongozo itakayopunguza vihatarishi vya uwekezaji katika sekta ya milki ili kuwapa wawekezaji uhakika wa mitaji.
Ameeleza kuwa taasisi za fedha zinazotoa mikopo ya nyumba zimeongezeka kutoka tatu zilizokuwepo awali hadi zaidi ya 29 kwa sasa, hatua inayopanua fursa za upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa miradi ya milki.
Ameitaja kampuni ya Tanzania Mortgage Refinance Company kuwa hatua muhimu katika kuimarisha soko la mikopo ya nyumba nchini.
Kuhusu mipango miji, Dk. Mwigulu amewataka wawekezaji, waendelezaji wa miradi ya milki na wananchi kuzingatia mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kuepuka ujenzi holela unaosababisha changamoto za upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.
Katika hatua nyingine, amesisitiza umuhimu wa sekta ya milki katika maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027, akieleza kuwa nchi inahitaji uwekezaji zaidi katika hoteli, nyumba za kupangisha na miundombinu mingine ya malazi ili kuwahudumia wageni watakaoingia nchini.
Awali, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, amesema wizara hiyo imeanza hatua za kuimarisha usimamizi wa sekta ya milki, ikiwemo mpango wa kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Sekta ya Milki ya Makazi (Real Estate Regulatory Authority – RERA), itakayoweka mwongozo na kusimamia shughuli za sekta hiyo nchini.



