Wananchi wanufaika matibabu ya macho bure Chanika

DAR ES SALAAM: WANANCHI wametakiwa kujitokeza kwa wingi kutumia huduma za matibabu ya macho zinazotolewa bure kupitia kambi maalumu ili kubaini mapema changamoto za macho na kupata matibabu kabla hali zao hazijawa mbaya zaidi.

Wito huo umetolewa na baadhi ya wananchi walionufaika na huduma za upimaji na matibabu ya macho katika kambi maalumu iliyofanyika katika Kituo cha Afya Chanika, jijini Dar es Salaam, iliyoandaliwa na Majey Foundation kwa kushirikiana na Lions Clubs International.

Wananchi hao wamesema huduma hizo zimekuwa msaada mkubwa kwao, hususan wale waliokuwa na changamoto za kuona lakini wakashindwa kupata matibabu kutokana na gharama za huduma za afya.

Mmoja wa wanufaika, Silika Siwale, amesema awali alikuwa na changamoto ya kuona iliyomfanya ashindwe kusoma vizuri, lakini baada ya kufanyiwa uchunguzi katika kambi hiyo amepatiwa miwani itakayomsaidia kuboresha uwezo wake wa kuona

.

Kwa upande wake, Said Kilumbi amesema aliamua kujitokeza baada ya kuona tangazo la huduma hizo za bure na kubaini kuwa alikuwa na tatizo kwenye jicho lililohitaji uchunguzi.

“Nimeona tangazo la huduma hii ya upimaji wa macho bure, nimekuja kupima na kubainika kuwa nina kinyama pembeni ya jicho. Hivyo nimepewa miwani. Nawashauri wengine wajitokeze kupata huduma hizi za bure,” amesema Kilumbi.

Akizungumzia kambi hiyo, Daktari Bingwa wa Macho kutoka Majey Foundation, Dk Majala Majala, amesema wameamua kuandaa huduma hizo kutokana na uhitaji mkubwa wa matibabu ya macho miongoni mwa wananchi.

Amesema changamoto za macho zinawakabili watu wa rika mbalimbali, kuanzia watoto hadi wazee, huku baadhi yao wakishindwa kupata matibabu stahiki kutokana na gharama na ukosefu wa uelewa kuhusu huduma zinazopatikana.

Ameeleza kuwa katika kambi hiyo wananchi wamepatiwa huduma mbalimbali zikiwemo upimaji wa macho, uchunguzi wa presha ya macho, upimaji wa kisukari, utoaji wa dawa na miwani pamoja na upasuaji wa mtoto wa jicho, zote zikitolewa bila malipo.

Naye Mratibu wa Lions Club, Ragib Hassanalli, amesema sehemu ya fedha zinazopatikana kupitia shughuli za uchangishaji, ikiwemo mbio za hisani zinazofanyika mwezi Januari, hutumika kurejesha huduma kwa jamii kupitia miradi mbalimbali ya kijamii.

Amesema kupitia utaratibu huo, wamekuwa wakishirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wananchi wenye changamoto za kiafya wanapata huduma wanazohitaji bila kikwazo cha gharama.

Aidha, amewashukuru wananchi waliojitokeza kupata huduma hizo, pamoja na uongozi wa Kituo cha Afya Chanika na Serikali kwa kuweka mazingira yanayowezesha wadau kushiriki katika utoaji wa huduma kwa jamii.

Waandaaji wa kambi hiyo wamesema wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuandaa kambi nyingine za matibabu ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wenye changamoto za macho.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button