Tamasha kulenga kukuza utalii wa ndani

ARUSHA; WADAU wa utalii nchini wamekuja na ubunifu mpya wa kukuza utalii wa ndani na burudani za kifamilia kupitia tamasha la Christmas Market, litakalofanyika kwa siku sita ndani ya wikiendi mbili mfululizo mwezi Desemba mwaka huu.
Tamasha hilo linalenga kuwakutanisha familia, wafanyabiashara na wajasiriamali katika kusherehekea sikukuu ya Krismasi, huku likitoa fursa ya kukuza biashara na kuongeza mzunguko wa fedha katika sekta ya utalii.
Linatakiwa kuongeza msisimko wa msimu wa sikukuu jijini Arusha kwa kuwapa wananchi na wageni fursa ya kufurahia burudani, mandhari yaliyopambwa kwa mapambo ya Krismasi, bidhaa mbalimbali pamoja na shughuli za kifamilia.
Mkurugenzi wa Kilifair Promotion Company Ltd, Dominic Shoo, amesema tamasha hilo litafanyika Desemba 11, 12 na 13, pamoja na Desemba 18, 19 na 20 katika Tanzanite Event Park, eneo la King’ori, Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha.
Amesema Christmas Market ni tamasha la kwanza nchini kufanyika kwa mtindo huo, likiwa na lengo la kuanzisha utamaduni mpya wa kusherehekea Krismasi kwa kuwakutanisha watu wa rika mbalimbali katika mazingira ya burudani, biashara na mapumziko ya kifamilia.



