Watanzania washuriwa kutumia fursa za kibiashara Dubai

DUBAI: Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amewataka Watanzania kutumia fursa za biashara zilizopo Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na kuthamini bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini ili kukuza biashara za ndani na kuongeza ushindani wa Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Wito huo umetolewa Novemba 28, 2026, jijini Dubai, UAE, wakati wa hafla ya utoaji wa Tuzo za Consumer Choice Awards Africa (CCAA), zilizotolewa kwa wafanyabiashara mbalimbali kutoka mataifa ya Afrika, ikiwemo Tanzania.
Londo amesema matumizi ya bidhaa za Made in Tanzania ni muhimu katika kuimarisha wafanyabiashara wa ndani, huku akieleza kuwa kufanyika kwa tuzo hizo Dubai kunatoa nafasi ya kuunganisha biashara za Afrika na masoko ya kimataifa, wawekezaji na washirika wa kimkakati.

Amesisitiza kuwa ubora wa bidhaa na huduma ni msingi wa kujenga uaminifu kwa wateja na kupanua masoko, akieleza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za Watanzania wanaochangia kukuza sekta binafsi ndani na nje ya nchi.
Amebainisha kuwa sekta binafsi inatarajiwa kuchangia asilimia 70 ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, hivyo umuhimu wa kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji ni mkubwa.

Aidha, amewakaribisha wawekezaji kutoka UAE na mataifa mengine kuwekeza Tanzania katika sekta za uchakataji wa mazao ya kilimo, uongezaji thamani wa madini, nguo, ngozi, dawa, usindikaji wa vyakula na uzalishaji viwandani.
Amesema Tanzania ina nafasi ya kijiografia inayoiwezesha kufikia masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Ameongeza kuwa kupitia Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya mwaka 2025 na Sera ya Taifa ya Biashara ya mwaka 2023, Serikali inalenga kuimarisha uzalishaji, kuongeza ushindani na kupanua fursa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.



