Wafuasi wa Bolsonaro mikononi mwa polisi

#KIMATAIFA: Polisi nchini Brazil wamewakamata waandamaji zaidi ya 300 waliovamia Bunge la Congress, Ikulu ya Rais na Mahakama ya Juu ambao wanamuunga mkono Rais wa zamani Jair Bolsonaro, kwa mujibu wa ripoti mbalimbali nchini humo.
Katika ‘tweet’ ya jana, polisi walisema watu hao wamezuiliwa katika mji mkuu, Brasilia, baada ya ghasia za maelfu ya wafuasi wa Bolsonaro ambao walikataa kukubali kushindwa kwake katika uchaguzi.

“Uchunguzi utaendelea hadi mhusika wa mwisho atambuliwe,” polisi waliahidi kwenye kauli yao.
Hakukuwa na ripoti za mara moja za vifo au majeruhi kutokana na vurugu hizo, lakini wavamizi hao walifanya uharibifu wa baadhi ya samani baada ya kuharibu madirisha ya ikulu ya rais na baadhi ya sehemu za Bunge na Mahakama ya Juu.
Machafuko hayo yaliyodumu kwa zaidi ya saa tatu, yalisisitiza mgawanyiko mkali ambao bado unaikumba nchi hiyo ikiwa ni siku chache tangu kuapishwa kwa Rais wa mlengo wa kushoto, Luiz Inacio Lula da Silva, aliyemshinda Bolsonaro katika uchaguzi wa Oktoba.

Katika mkutano na wanahabari kutoka jimbo la Sao Paulo, Lula alimshutumu Bolsonaro kwa kuhimiza ghasia za wale aliowaita “washirikina wa kifashisti,” na kusoma amri mpya iliyotiwa saini kwa serikali ya shirikisho kuchukua udhibiti wa usalama huko Brasilia.
“Hakuna mfano wa walichokifanya,” Lula alisema. “Watu hawa wote waliofanya hivi watapatikana na wataadhibiwa.” Baada ya hapo alienda Brasilia kuzuru majengo yaliyoharibiwa na kusimamia majibu, TV ya Brazili Globo iliripoti.
Rais wa Marekani, Joe Biden aliyataja matukio hayo kuwa “mashambulio dhidi ya demokrasia na uhamishaji wa madaraka kwa amani,” akiongeza kuwa taasisi za kidemokrasia za Brazil ziliungwa mkono kikamilifu na Washington.
Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel alituma ujumbe wa “kulaani kwake kabisa”, na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitaka kuheshimiwa kwa taasisi za Brazil na kumtuma Lula “uungwaji mkono usio na shaka wa Ufaransa”.

Rati ya viongozi wa Amerika ya Kusini walizungumza, huku Rais wa Chile, Gabriel Boric akilaani “mashambulizi ya woga na mabaya dhidi ya demokrasia” na Andres Manuel Lopez Obrador wa Mexico aliita “jaribio la mapinduzi la kulaumiwa”.
Wabunge kadhaa wa Kidemokrasia nchini Marekani wakati huo huo walisema Washington haiwezi tena kutoa “kimbilio” la Bolsonaro nchini humo.
“Lazima tusimame katika mshikamano na serikali ya Lula iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia,” mbunge wa Congress Alexandria Ocasio-Cortez alitweet. “Marekani lazima ikome kutoa kimbilio kwa Bolsonaro huko Florida.”



