Mama Maria Nyerere atunukiwa ‘Malkia wa Nguvu’ mwaka 2023

MKE wa aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere ametunukiwa tuzo ya Malkia wa Nguvu ya mwaka huu.

Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson alikabidhi tuzo hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere ambaye ni mtoto wa mama Maria Nyerere.

Tuzo hizo za Malkia wa Nguvu zilitolewa Dar es Salaam juzi usiku kuthamini mchango wa wanawake kwenye masuala tofauti ya maendeleo.

Tuzo ya Uongozi imekwenda kwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji, Anna Makakala.

“Namshukuru mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini pamoja na viongozi wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kunipa ushirikiano katika kazi zangu za kila siku za kukitumikia taifa” alisema Kamishna Jenerali Makakala baada ya kupokea tuzo hiyo.

Mshindi wa tuzo ya Uongozi wa Biashara, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji na biashara nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Somoe Ismail amepata Tuzo ya Funguo ya maisha kwa kuwashika mkono malkia wengine katika eneo lake la kazi.

Tuzo ya Ubunifu na uvumbuzi ilikwenda kwa Tasila Melita ambaye amebuni mashine ya kuteketeza taulo za kike zinazotumika wakati wa hedhi.

Tuzo ya Ustawi wa Jamii imenyakuliwa na Dk Stella Rwezahura ambaye ni Daktari Bingwa wa Damu ambaye ndiye alisimamia upandikizwaji wa uloto kwa wagonjwa 11 wenye saratani ya damu nchini.

Wengine waliopata tuzo ni Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundatin, Tuli Ester Mwambapa aliyepata tuzo ya mhamasishaji bora wa mwaka.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button