Vikundi 28 Iringa Mjini vyalamba Sh milioni 402

IRINGA: Ndoto za mamia ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Manispaa ya Iringa za kujikwamua kiuchumi zimeendelea kupata uhai baada ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kukabidhi mikopo ya Sh milioni 402.26 kwa vikundi 28 vilivyokidhi vigezo, huku Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, akitekeleza ahadi ya Sh milioni moja kwa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Kusikia mkoani Iringa.
Hafla hiyo, iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, imekuja wakati Serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ikiendelea kusisitiza uwezeshaji wa wananchi kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, hatua inayotarajiwa kuongeza ajira, kukuza biashara ndogo na kuimarisha uchumi wa kaya.
Mbali na vikundi hivyo kukabidhiwa hundi za mikopo, Mbunge Ngajilo alikabidhi Sh milioni moja taslimu kwa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Kusikia, akitimiza ahadi aliyoitoa mbele ya wananchi wakati wa mkutano wa hadhara ulioongozwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, uliofanyika hivi karibuni mjini Iringa.
Hatua hiyo ilipokelewa kwa furaha na wanachama wa chama hicho, wakisema msaada huo utawasaidia kushiriki mkutano wao wa kitaifa unaotarajiwa kufanyika mjini Tanga baadae mwaka huu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ngajilo alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha fedha za mikopo zinakuwa mtaji wa kuondoa umaskini badala ya kubaki kwenye akaunti za halmashauri.

“Tunataka fedha hizi ziwafikie wananchi, ziongeze mitaji ya biashara na zijenge uchumi wa familia. Tunawaomba wanufaika wazitumie kama zilivyokusudiwa na wazirejeshe kwa wakati ili na wengine wanufaike,” alisema.
Alibainisha kuwa, licha ya Manispaa ya Iringa kutokuwa na mapato makubwa ikilinganishwa na baadhi ya halmashauri nchini, imeendelea kutekeleza kwa ufanisi agizo la Serikali la kutenga fedha kwa ajili ya mikopo ya makundi maalumu.
Ngajilo alisema hatua hiyo inaendana na uamuzi wa Bunge uliopitisha ongezeko la fedha za mikopo ya makundi maalumu kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15 ya mapato ya ndani ya halmashauri, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za uwezeshaji kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026 halmashauri imefanikiwa kutoa jumla ya Sh bilioni 1.202 kupitia fedha za marejesho na mchango wa asilimia 10 ya mapato ya ndani.
Alisema katika bajeti ya mwaka huo, halmashauri ilitenga Sh milioni 793.67 kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu awamu ya kwanza, lakini kutokana na marejesho mazuri ya mikopo ya awali, kiasi kilichotolewa hadi kufikia Machi 2026 kilifikia Sh milioni 799.99, kikinufaisha vikundi 69 vyenye wanachama 330, wakiwemo wanaume 67 na wanawake 263.
Katika awamu ya sasa, alisema vikundi 28 vimekabidhiwa jumla ya Sh milioni 402.26, ambapo wanawake wamepata Sh milioni 152.50, vijana Sh milioni 153.36, na watu wenye ulemavu Sh milioni 96.40.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamiii Manispaa Mwatum Dossi alisema mafanikio hayo yametokana na mchakato madhubuti wa uhakiki uliohusisha Kamati za Huduma za Mikopo ngazi ya kata, Halmashauri, Menejimenti na Kamati ya Uhakiki ya Wilaya.

Alifafanua kuwa vikundi vilivyofanikiwa vilithibitisha kuwa na miradi yenye tija, maeneo ya kufanyia shughuli, nyaraka muhimu za biashara zikiwemo TIN, leseni na mikataba ya upangishaji, pamoja na mifumo mizuri ya utunzaji wa kumbukumbu.
Hata hivyo, alisema jumla ya vikundi 49 vilivyoomba mikopo yenye thamani ya Sh w
Milioni 782.79 havikupata fedha hizo baada ya kushindwa kukidhi masharti yaliyowekwa.
Kwa mujibu wa Dossi, baadhi ya vikundi vilionyesha miradi isiyo yao, vingine havikuwa na maeneo ya kuendeshea shughuli, vilikosa nyaraka muhimu za biashara au vilishindwa kupata alama za ufaulu zilizowekwa kwenye tathmini.
Aliwataka waombaji ambao hawakufanikiwa kurekebisha kasoro zilizobainika ili waweze kupata fursa katika awamu zinazofuata.
Akihitimisha hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, aliwataka wanufaika kuiona mikopo hiyo kama mtaji wa maendeleo na si fedha za matumizi ya kawaida.
Alisema kurejesha mikopo kwa wakati kutahakikisha wananchi wengi zaidi wanaendelea kunufaika na mpango huo, huku akiipongeza Manispaa ya Iringa kwa kusimamia kwa uwazi na uadilifu mchakato mzima wa utoaji wa mikopo.
Sitta pia alimpongeza Mbunge Fadhili Ngajilo kwa kuanza kutekeleza ahadi aliyoitoa kwa watu wenye ulemavu wa kusikia, akisema utekelezaji wa ahadi kwa vitendo huongeza imani ya wananchi kwa viongozi wao na kuimarisha ushirikiano katika kuleta maendeleo.



