Taasisi yahamasisha uwekezaji katika kilimo

Taasisi ya Kusaidia Sekta Binafsi ya Kilimo (PASS Trust), imezindua rasmi katika ukanda wa nyanda za juu kusini mjini kampeni yake ya Kijanisha Maisha kwa kilimo endelevu, inayolenga kuchochea uwekezaji katika miradi inayozingatia ajenda ya Ukuaji wa Kijani Shirikishi katika kuhamasisha uwekezaji katika kilimo endelevu na uchumi wa mzunguko.

Tangu kuanza kwa mradi huo wa Ukuaji wa Kijani Shirikishi mwaka 2021 hadi Desemba 2022, PASS Trust imesema zaidi ya wanufaika 516,000 nchi nzima ambao kati yao asilimia 71 ni wanawake tayari wamenufaika na udhamini wa mikopo ya kilimo biashara ya hadi asilimia 80 uliotolewa taasisi hiyo.

“Hadi sasa PASS Trust ni taasisi ya kipekee nchini ambayo inafanya kazi kama moja ya mifuko iliyopo chini ya Baraza la Taifa la uwezeshaji wananchi Kiuchumi (NEEC), ambayo imeamua kujikita kwenye shughuli za udhamini wa mikopo ya kilimo biashara kupitia taasisi mbalimbali za kifedha nchini na kuwajengea uwezo wanaojihusisha na kilimo biashara,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa PASS Trust, Yohane Kaduma wakati akitoa taarifa hiyo.

Alitoa taarifa hiyo mjini Iringa leo kwenye mkutano wa mashauriano na wadau mbalimbali juu ya kuhamasisha uzalishaji unaozingatia ajenda hiyo inayolenga kilimo endelevu kitakachotosheleza mahitaji ya kujikimu, biashara na kuhakikisha usalama wa chakula cha uhakika na kilimo stahimilivu.

“PASS Trust ina mchango mkubwa katika kuchochea na kuwezesha ukuaji wa kilimo nchini tangu kuanzishwa kwake miaka 23 huku tukitoa kipaumbele kwa vijana na wanawake ambapo tunawapa dhamana ya mikopo kupitia benki 14 tunazoshirikiana nazo na huduma za maendeleo ya biashara ili kufikia malengo yao,” alisema.

 

Alisema tangu kuanzishwa kwa PASS Trust, jumla ya biashara zipatazo 66,077 zilinufaika na dhamana za udhamini wa mikopo ya kilimo biashara kutoka taasisi hiyo na kuwafikia takribani wanufaika milioni 3.4 ambao kati yao asilimia 51 ni wanawake huku ajira zipatazo milioni 2.7 zikitengenezwa nchi nzima.

“Hata hivyo Katika kanda hii ya nyanda za juu kusini inayojumuisha mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe pamoja na mkoa wa Rukwa, tumeweza kuwafikia zaidi ya wajasiriamali milioni moja wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kilimobiashara katika sekta za mazao, mifugo, mazao ya misitu pamoja na wasindikaji,” alisema na kuongeza kwamba PASS Trust inatoa huduma katika mikoa yote nchini kwa kupitia ofisi zake za kanda.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego alitoa pongezi kwa PASS Trust kwa kuja na mpango wa kukuza uchumi kupitia ajenda ya Ukuaji wa Kijani Shirikishi, akisema ni njia bora ya kuchochea kilimo endelevu.

“Naipongeza PASS Trust kwa ubunifu na kuanzisha ajenda ya Ukuaji wa Kijani Shirikishi ambayo kwa hakika inachochea maendeleo endelevu ya kiuchumi yanayoenda sambamba na utunzaji wa mazingira na kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo,” alisema na kuongeza kuwa inawawezesha wakulima kujihusisha kikamilifu na kilimo biashara kwa namna inayojumuisha jamii nzma.

Aliishukuru serikali ya Denmark kwa ufadhili wake mkubwa kwa PASS Trust akisema unarahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha na maendeleo ya biashara kwa wafanyabiashara wa kilimo nchini na umesaidia kwa kiasi kikubwa wakulima wengi ambao wamegawanyika katika makundi matatu ya watu binafsi, vikundi na makampuni.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button