Maboresho Hospitali ya Amana yavuta wengi

HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa ya Amana iliyopo Dar es Salaam inapiga hatua mbalimbali katika kutoa huduma kwa jamii. Amana iliyoanzishwa mwaka 1954 imepitia hatua mbili kabla ya kufikia hatua hiyo ya sasa ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Dk Gilbert Kwesi anasema mwaka 1982 ilipandishwa hadhi kuwa Kituo cha Afya, miaka nane baadaye mwaka 1990 ilipandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya na baadaye mwaka 2010 kupitia Gazeti la Serikali ilitangazwa rasmi kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

“Utaona tangu ilipoanza ilianza ikiwa changa ikitoa huduma za msingi kabisa za afya, lakini sasa hivi tunaongea utoaji wa huduma za kibingwa na sasa tunaelekea katika hatua ya kutoa huduma za kibingwa bobezi.

“Kwa hiyo ni hatua kubwa ambayo hospitali imepiga tangu 1954 ilipoanzishwa mpaka leo hii 2023, kwa wastani hospitali inapokea wagonjwa wa nje wapatao 500 kwa siku,” anasema Dk Kwesi.

Anasema kwa wastani robo mwaka wanapokea wagonjwa wasiopungua 45,000. “Na siku za karibuni tumeona ongezeko kubwa la wagonjwa ambao kutoka hiyo 45,000 ambayo tulizoea katika robo mwaka zilizopita mpaka kufikia hii robo ya mwisho ambayo tumeimalizia, tumepokea wagonjwa 55,000.

Unaweza ukaona ongezeko hilo la zaidi ya wagonjwa 10,000,” anasema Dk Kwesi. Kwa maelezo ya Dk Kwesi kwa wastani hospitali hiyo inalaza wagonjwa kati ya 50 mpaka 80 kwa siku na ina uwezo wa vitanda 350. “Lakini isivyo bahati kwa ongezeko hili nililolitaja linazidi uwezo wa hospitali. Kwa wastani kwa sasa hivi tunavyoongea leo tuna wagonjwa wasiopungua 400.

“Na kwa wastani ukilinganisha na sensa ya 2012 na sensa ya 2022 kuna ongezeko kubwa la wagonjwa. Kwa sasa kwa mujibu wa sensa ya mwaka jana, hospitali inahudumia wagonjwa wapatao milioni 1.5 kwa mwaka kwa eneo la Amana,” anasema.

Anasema wanahudumia watu kutoka nchi mbalimbali na Watanzania kutoka mikoa mbalimbali na imekuwa ikipokea wagonjwa wa rufaa na wasio wa rufaa kwa hiyo ukiacha hiyo milioni 1.5, bado kuna wagonjwa wengine wanahudumiwa nje ya eneo hilo la Amana.

Dk Kwesi anasema kwa ujumla wanahudumia zaidi ya watu milioni 1.5. Anakiri mwaka jana kumekuwa na mapinduzi makubwa katika huduma za afya kwani awali hospitali hiyo ilitoa baadhi ya huduma na nyingine zilikuwa hazijaanza kutolewa.

Anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza mapinduzi hayo yaliyowezesha hivi sasa hospitali hiyo kutoa huduma za CT Scan, huduma za wagonjwa mahututi lakini pia huduma za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo. “Kwa hiyo huduma zote hizi kupitia mradi wa IMF chini ya serikali zinatolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana.

Lakini tumeboresha sana huduma nyingine za magonjwa ya dharura kiasi kwamba mgonjwa anapofika katika hali ya dharura hii ndio sehemu pekee ambapo mgonjwa anaokolewa au asiokolewe. “Kwa hiyo kuimarisha kitengo hiki kumefanya wagonjwa wengi wanakuja katika hali mbaya waliopata ajali na magonjwa mbalimbali wameokolewa katika kitengo hiki,” anasema Dk Kwesi.

Anasema pamoja na mafanikio hayo kuna changamoto mojawapo inasababishwa na ongezeko la wagonjwa na kwamba hospitali hiyo imekuwa ni kivutio kwa wateja walioko ndani na nje ya Ilala, hivyo ongezeko hilo linafanya hospitali ielemewe na huduma.

Pia nyingine ni ufinyu wa bajeti, kwani tangu hospitali hiyo imejengwa kuna mabadiliko machache kwenye miundombinu kutokana na ufinyu wa bajeti. Anaeleza ufinyu wa eneo ni changamoto nyingine wanayokabiliana nayo hivyo wanahitaji kupanuka.

Dk Kwesi anasema mwaka 2010 hospitali ilikuwa na madaktari bingwa wanne tu lakini sasa hawapungui 30. “Kwa maana hiyo huduma zinatolewa katika maeneo mbalimbali ni za upasuaji, uzazi, watoto na nyingine za kibingwa zikiwemo za macho na masikio, sasa ongezeko la Inatoka 9 ‘Bajeti mwaka huu imejali mrengo … huduma hizo zinatakiwa kuendana na ukubwa wa eneo na miundombinu iliyopo. “Katika eneo hili tunaomba taasisi Amana iangaliwe kwa jicho la kipekee, ni hospitali pekee na kubwa katika eneo la Ilala.

Idadi ya wateja wanaopokelewa na huduma zinazotolewa kimsingi hospitali inatakiwa kuongezewa eneo,” anasema. Anasema umekuwepo mchakato wa muda mrefu wa kuomba eneo la mbele la hospitali hiyo, lakini umekuwa mgumu kwa miaka mingi. Ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa fedha, Oktoba mwaka huu watafanya harambee kukusanya fedha kupandisha jengo la wazazi ili kupokea wagonjwa wengi zaidi.

“Kwa sasa hivi hali ni mbaya kwa sababu kuna wakati wagonjwa wakiwa wengi wanalazimika hata kulala wawiliwawili kitu ambacho si kizuri,” anasema Dk Kwesi. Anakaribisha wadau kuchangia maendeleo ya wananchi kupitia hospitali hiyo kwa kuwa haiwezi kujiendesha yenyewe bila kuwa na wadau.

Historia hiyo ya Amana ilibainika wakati taasisi ya ZamZam ilipotoa msaada kwa hospitali hiyo kwa kuwapatia viti 10 vya magurudumu vya kubebea wagonjwa katika siku za karibuni ambapo mgeni rasmi Naibu Spika na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu alipokea msaada huo. Zungu alisema gharama za hospitali bado zipo juu wakati mitambo yake imenunuliwa na serikali, umeme unalipwa na serikali na wataalamu wanafundishwa na serikali.

Anasema yote hiyo ni kwa sababu mitambo inatoka nje ya nchi hivyo inabidi ibadilishwe mitambo inayouzwa kwa gharama za juu ili iwekwe ya gharama nafuu wagonjwa waweze kupata unafuu. Lakini anasema naye amekuwa akifuatilia kwa nguvu zote ili Amana iongezewe eneo lililopo mbele ya hospitali hiyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button