Tuwachangie vifaa vya ujenzi Hanang

HANANG, Manyara: SERIKALI inatoa wito kwa wanaowiwa kutoa misaada kwa waathirika wa maafa ya Hanang, kujikita zaidi katika kutoa misaada ya vifaa vya ujenzi.

 

Hayo yameelezwa katika taarifa ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi kuhusu taarifa ya Serikali juu ya maendeleo ya hali baada ya maafa yaliyotokea wilayani Hanang Mkoa wa Manyara. na kueleza kuwa, Serikali imeendelea kupokea na kugawa misaada ya chakula na mahitaji muhimu kwa waathirika wa maafa ya Hanang mkoani Manyara.

“Serikali inawashukuru Watanzania kwa utu, upendo, uzalendo na moyo wa kujitolea ambao umesaidia kupatikana kwa chakula cha kutosha na mahitaji muhimu ili kuwasaidia waathirika kuendelea na maisha yao,” imeeleza taarifa hiyo.

Hadi sasa misaada ya chakula na mahitaji muhimu imefikia thamani ya sh. 2,583,306,997.00 na fedha taslimu shilingi 5,208,729,711.00. Fedha taslimu zinajumuisha shilingi bilioni 2.5 zilizoletwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na shilingi 2,708,729,711.00 zilizomo kwenye akaunti ya Mfuko wa Taifa wa Misaada ya Maafa inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

 

“Kati ya fedha hizo, kiasi cha sh. 2,289,260,025.00 zimechangwa na taasisi na mashirika ya umma kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na kiasi kilichobaki cha sh. 419,469,152.00 kimechangwa na wahisani mbalimbali,” imeeleza taarifa hiyo.

Serikali ilianza kugawa chakula cha kutosha siku 30 na mahitaji mengine muhimu kwa waathirika kwenye kambi tatu huku ikiwasaidia kuungana na ndugu zao.

 

Kambi hizo tatu sasa zimefungwa baada ya waathirika wote 690 kutoka kaya 140 kurejea makwao na kwa ndugu zao. Waathirika 534 walikuwa wakilala kambini na 156 walikuwa wakija asubuhi na kuondoka jioni.

 

Utaratibu wa kugawa misaada hiyo unaoratibiwa na Idara ya Maafa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikishirikiana na uongozi wa mkoa wa Manyara na wilaya ya Hanang pamoja na kamati zao za usalama, unatumia watalaam kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Mgawo wa misaada hii unalenga kwanza waathirika 1,292 waliothibitika kupoteza nyumba zao ama kuharibika au kuingia tope.

Idadi hii ilipatikana baada ya tathmini ya kina ya picha za satelaiti, rekodi za sensa, ukaguzi halisi wa nyumba hadi nyumba na rekodi za serikali za mitaa katika ngazi ya vitongoji, vijiji na kata.

 

Utaratibu wa ugawaji misaada umewekwa kwa kubandika majina ya waathirika kwenye ofisi za kata baada ya kukamilika kwa tathmini ambapo mhusika akifika huelekezwa kituo chake cha kupokelea misaada. Tangu wiki iliyopita wananchi wamekuwa na ratiba za kwenda kupokea misaada kila siku kutokana na wingi wa misaada hiyo.

 

Kwa wastani kila kaya inapata chakula cha kutosha miezi sita au zaidi ambapo kwa baadhi ya bidhaa kama sukari wananchi hao wanapewa ya kutosha kutumia kwa zaidi ya miaka miwili kwa mujibu wa vipimo vya lishe.

Misaada inayotolewa ni chakula cha mahindi, ngano, mchele, unga wa mahindi, unga wa ngano, maharage, mafuta ya kula, maziwa, unga wa lishe kwa watoto, mayai, sabuni, magodoro, mablanketi, mashuka, mikeka, ndoo, majiko ya kupikia ya gesi na mitungi yake, masufuria, nguo, viatu, kandambili na vingine vingi.

 

Idadi ya watu waliopoteza maisha imebakia kuwa 89 tangu tarehe 11 Desemba na mwili mmoja wa mtoto wa kike bado haujatambuliwa. Maafa haya yalitokea alfajiri ya tarehe 3 Desemba, 2023, baada ya maporomoko ya tope, mawe, magogo na maji kutoka mlima Hanang kuvamia vijiji vinne vilivyokuwa kando ya mlima Hanang na kata nne za mji mdogo wa Katesh wilayani Hanang.

Hadi sasa majeruhi wanne bado wanatibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara iliyopo mjini Babati na mmoja amepelekwa Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma. Serikali imegharamia matibabu, mazishi na kutoa mkono wa pole kwa wafiwa. Majeruhi wote walifikia jumla ya 139.

 

Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa akaunti ya kielektronikia kuchangia fedha za misaada yenye nambari 9921159801 iliyopo Benki Kuu ya Tanzania na inayopokea fedha kupitia benki yoyote nchini na pia kutoka nje ya nchi kwa kutumia swift code ya TANZTZTX. Miamala yote inatakiwa kuwa na maelezo MAAFA HANANG.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button