Uwekezaji wakua kwa asilimia 60 nchini
KITUO Cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimebainisha, kutungwa kwa sheria mpya ya uwekezaji ya mwaka 2022 imechagiza ongezeko la usajili wa miradi mipya kwa zaidi ya asilimia 60 ndani ya mwaka mmoja.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri amebainisha hayo mbele ya waandishi wa habari mjini Geita ikiwa ni muendelezo wa ziara ya TIC kuhamasisha dhana ya uwekezaji wa ndani.
Amesema sheria ya uwekezaji ya mwaka 2022 ilitungwa mahususi kwa ajili ya kuwezesha watanzania wenye mitaji na wanaotamani kuanza kuwekeza waweze kunufaika na mazingira rafiki ya uwekezaji.
“Yale mambo ambayo walikuwa wanashindwa kuyafanya kabla ya mwaka 2022 sheria ya uwekezaji imewarahisishia, kwa mtanzania yeyote kutokana na uwekezaji anatamani kuufanya aje TIC aulize.”
Amesema sheria hiyo na mazingira rafiki ya uwekezaji chini ya serikali ya awamu ya sita imechagiza ongezeko hilo kutoka kusajili miradi 273 mwaka 2022 hadi kufikia kusajili miradi 504 kwa mwaka 2023.
“Lakini kubwa kuliko yote katika miradi iliyoongezeka mwaka 2023 takribani nusu ni miradi ya watanzania ingali mwaka 2022 miradi ya watanzania ilikuwa kati ya asilimia 20 na 30.
“Tumeona kuwa kuna umma wa watanzania wanajua, lakini pia kama wana mwamko hawa wachache tukiwafikia wengi zaidi kwa taarifa tutaamusha na wenyewe hali yao waweze kuwekeza.”
Gilead ametaja baadhi ya sekta zenye mwamko mkubwa wa uwekezaji ni sekta ya viwanda, kilimo, uchukuzi, madini, utalii na sekta ya ujenzi.
“Mwaka jana (2023) tumesajili miradi hiyo 504 yenye mitaji takribani dola bilioni 5.6 hizi ni zaidi ya trilioni 11 za kiuwekezaji zinazotarajiwa kuleta zaidi ya ajira laki moja kwa watanzania.
“Ukilinganisha na mwaka 2022 ambao tulikuwa na uwekezaji wa takribani Dola bilioni 3 ingali kwa mwaka 2021 kulikuwa na uwekezaji wa takribani dola bilioni mbili pekee.”



