Dorothy Semu: Nitatimiza malengo ACT
MAKAMU Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo Bara, Dorothy Semu amesema anaamini katika uongozi wa pamoja, utumishi wa watu na kuonyesha njia ili kutimiza kwa ukamilifu malengo makubwa ya chama cha ACT Wazalendo.
Dorothy amesema hayo jana Februari 18 2024 alipochukuwa fomu kugombea nafasi ya kiongozi wa chama hicho iliyokaliwa na Zitto Kabwe kwa muda mrefu.

Katika taarifa yake kwa umma, Dorothy ambaye ni Waziri Mkuu Kivuli wa ACT Wazalendo amesema alipokuwa Katibu Mkuu 2017-2020 alikivusha chama hicho kwenye mawimbi ukandamizaji wa kidemokrasia, mawimbi ya kufutiwa usajili na kuvunja rekodi za usimamizi wa kifedha na kuwa chama kinachokua kwa kasi kuliko vyote Afrika.
“Nikiwa Makamu Mwenyekiti Bara mwaka 2021 nilipewa jukumu jingine la kukaimu uenyekiti wa chama baada ya kutangulia mbele za haki kwa aliyekuwa mwenyekiti wetu mpendwa Maalim Seif”.

Sambamba na hilo, Dorothy amesema anaamini katika wajibu mkubwa wa vyama shindani, uwepo wa chama hiko katika siasa za vyama vingi umeendelea kutoa tafsiri halisi ya nini wajibu wa vyama vya siasa katika siasa za ushindani na kuleta sera za kimapinduzi za kubadilisha hali ya umaskini.
“Ninataka nafasi hii ya kiongozi wa chama kuendeleza dhima hii ambayo chama cha ACT Wazalendo imeibeba kwa miaka kumi sasa na matumaini inayotoa katika uongozi wa nchi yetu”. ameongeza Semu.



