Kasi yatakiwa usajili vyama vya ushirika

NAIBU Waziri wa Kilimo, David Silinde ameiagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), kuongeza kasi ya kusajili vyama vya ushirika kwa kuwa ni njia pekee ya kumsaidia mkulima kuondokana na changamoto zinazomkabili za masoko na uhakika wa bei.

Silinde ametoa agizo hilo wakati akifungua maonesho ya Samia Kilimo Biashara Expo 2024 awamu ya tatu Wilayani Gairo, Mkoa wa Morogoro.

“Kupitia maonesho haya niwaagize Tume ya Maendeleo ya Ushirika muendelee kusajili kwa wingi Vyama vya Ushirika ili kumsaidia mkulima kutatua changamoto ya masoko, upatikanaji wa pembejeo na bei ya uhakika ya mazao,”amesema Silinde.

Pia amewataka wakulima nchini kuendelea kujiunga na vyama vya ushirika ikiwa na kutumia mfumo wa Stakabadhi za Ghalani kwa sababu ndio mkombozi wao kwenye ya kilimo.

“Niendelee kuwahimiza wakulima kutumia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa kutumia mfumo wa soko la BidhaaTanzania ili kupata bei za ushindani kwa mazao  na  kuongeza kipato chao,” amesema Silinde .

Naye Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabir Makame amesema wilaya hiyo ni ya kilimo na asilimia 95 ya wananchi wake wanajishughulisha na kilimo na wengine wamejiajiri katika sekta ya mifugo na biashara.

Makame amesema licha ya uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na mifugo, kumekuwa na kiwango kidogo cha uchakataji na uongezaji wa thamani hivyo mazao mengi kuuzwa nje ya wilaya kama  malighafi.

SOMA: Silinde: Watafiti wa kilimo ongezeni kasi

Amesema kuanzishwa kwa maonesho hayo  yanalenga kuwashsirikisha wakulima wengi ngazi ya kijiji na kata ili wapatiwe elimu bora ya uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo kwa tija na wataalamu mbalimbali wakiwemo wa sekta za kilimo, mifugo  na uvuvi .

“ Wengi wa wakulima hawa hushindwa kusafiri kwenda kwenye maonesho ya Kilimo , Mifugo  na Uvuvi  maarufu kama nanenane  ya kanda ya Mashariki ambayo huwa yanafanyika kwenye Viwanja wa Julius Kambarage Nyerere hapa Morogoro,” amesema Makame.

Makame amesema  tangu kuanzishwa kwa maonesho hayo yameleta matokeo chanya kwa wakulima kubadili mfumo ya kilimo kutoka cha mazoea na  kwenda katika matumizi ya kilimo cha kisasa.

Kwa upande wake Naibu Mrajis ( Uhamasishaji), Consolata Kiluma, amesisitiza  matumizi ya Mifumo ya kidigitali ya ununuzi kupitia Vyama vya Ushirika kupitia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX),pamoja na Mfumo wa Stakabadhi za ghala(WRRB) ili wakulima waweze kuwa na uwazi na uhakika wa bei ya mazao yao.

Kiluma amesema Tume hiyo  inaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waone umuhimu wa kujiunga na Vyama vya ushirika na matumizi ya mfumo wa kidigitali.

“Tunahamasisha matumizi ya mizani ya kidigitali  na  kupitia Vyama vya Ushirika ili changamoto ya mkulima kupunjwa bei ya mazao yao ikomeshwe na tayari tumeshafanikiwa katika baadhi ya mikoa na mkoa wa Morogoro ukiwemo” amesema Kiluma.

SOMA: Silinde amshukuru Samia miradi ya maendeleo

Mmoja wa mkulima na mkazi wa Gairo , Amina Semwenda amesema  mfumo wa stakabadhi ghalani ni mzuri , na kuomba elimu zaidi iweze kutolewa ikizingatiwa umuhimu wake kwenye  kumkomboa mkulima.

“ Ni mfumo mzuri unalinda  bei ya soko lakini kwa baadhi ya wakulima  bado elimu hiyo hawana na pia  hajajiunga na vyama vya Ushirika” amesema  Semwenda.

Habari Zifananazo

Back to top button