Onesho laingiza pato sekta ya utalii

TANZANIA imeendelea kupata mafanikio chanya kwenye sekta ya utalii kupitia onesho la Swahili International Tourism Expo (S!TE 2024 ) lilohitimishwa na wanunuzi 120 wa bidhaa za utalii kutoka nchi mbalimbali.
Akizungumza na wanahabari leo Oktoba 13, 2024 mara baada ya kufunga onesho hilo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi, Dk Pindi Chana amesema mwitikio umekuwa mkubwa kutokana na jitihada za Raisi Samia Suluhu Hassan katika kuitangaza The Royal Tour.
SOMA: Sekta ya utalii yasifiwa kuongeza pato la taifa
“Sekta ya utalii umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa kuanzia mtalii anavyoshuka airport,tax anavyochukua na hoteli mpaka anapopata wasaha wa kutembelea vivutio vya utalii nchini,”amesema Dk Chana.
Aidha amesema ulinzi wa rasilimali za Tanzania ikiwemo Misitu na mbuga za wanyama ni muhimu sana kwa taifa na kipaumbele kwa kila mtu ili kuendelea kustawisha uchumi wa nchi hivyo watanzania wanapaswa kuzitunza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania, Balozi Dk Ramadhan Dau amesema mafanikio waliyopata kwa mwaka huu ni ishara tosha ya mafanikio ya maandalizi ya onesho lijalo ambapo kwa mwaka huu limefanyika kwa mara ya nane tangu lilipoanzishwa mwaka 2014.



