Sekta ya utalii yasifiwa kuongeza pato la taifa

NAIBU Waziri ,Wizara ya Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula amesema sekta ya utalii imekuwa na mchango mkubwa kwenye ajira za Watanzania na pato la taifa.

Waziri Dunstan amesema hayo ni matokeo ya juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kufungua utalii kwa kuvitangaza vivutio hapa nchini ambapo imepelekea ongezeko la watalii.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar Es Salaam katika mkutano wa Jukwaa la Kitaifa la Uwekezaji kupitia utalii ambalo limefanyika leo Oktoba 12,2024 likienda sambamba na Onesho la Swahili International Tourism Expo (S!TE) katika ukumbi wa Mlimani City ,Naibu Waziri huyo amesema juhudi hizo zimepelekea pia kuwepo kwa mkutano huo uliowakutanisha wadau mbalimbali ikiwemo wawekezaji sekta ya Utalii.

Advertisement

“Mkutano huu ni muhimu kwani umehusisha pia watu wanataka kuwekeza katika sekta ya Utalii ikiwemo wa mahoteli na tumekuja hapa kujadiliana fursa zilizopo nchini,” amesema.

Amesema mkutano huo wa uwekezaji katika sekta ya utalii ambao unafanyika kando ya Onesho la S!TE 2024 ni dhihirisho na hakikisho kwa wawekezaji mbalimbali wa ndani na wa kimataifa kupitia utalii kuwa Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza ambapo asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni hapa nchini huchangiwa na sekta ya utalii.

“Kupitia mkutano huu pia tumewambia Watanzania na wawekezaji kuwa kufuatia mazingira mazuri yaliyowekwa na serikali Kwa mabenki hapa nchini sasa wanaweza pia kupata mikopo na kufanya Uwekezaji katika Utalii kupitia mabenki hayo kwani kwa sasa kuna sera rafiki za uwekezaji”amesema.

1 comments

Comments are closed.