Waziri Mkuu wa Burkina Faso atimuliwa kazi
KIONGOZI wa kijeshi wa Burkina Faso, Ibrahim Traoré, amemfukuza kazi Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Kyelem de Tambela na kuvunja serikali, tangazo la amri ya Rais limesema leo.
De Tambela alihudumu kama mkuu wa serikali tatu mfululizo, akivuka changamoto za mabadiliko kadhaa ya baraza la mawaziri.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ufaransa-AFP, hata hivyo, hakuna sababu rasmi iliyotolewa ya kuondolewa kwake.

Aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu Oktoba 2022 kufuatia mapinduzi yaliyomleta madarakani, Ibrahim Traoré.
Amri ya rais imetangaza kuwa “majukumu rasmi ya waziri mkuu yamekoma,” na imeeleza kuwa viongozi wa serikali iliyovunjwa wataendelea kushughulikia masuala ya sasa hadi serikali mpya itakapoundwa.”
Burkina Faso imekumbwa na hali ya kutokuwa na utulivu mkubwa tangu mapinduzi ya Januari 2022, wakati Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba alipochukua madaraka.
Chini ya mwaka mmoja baadaye, Damiba aling’olewa madarakani na Traoré, ambaye sasa anaongoza utawala wa kijeshi.
Damiba, ambaye alimng’oa madarakani Rais aliyechaguliwa Roch Marc Christian Kaboré, sasa yuko uhamishoni nchi jirani ya Togo.
Chini ya utawala wa sasa wa kijeshi, Burkina Faso imeweka kipaumbele katika kurejesha mamlaka ya kitaifa na mara kwa mara hukosoa mataifa ya Magharibi.


