UDSM Marathon kuboresha maisha ya wanafunzi
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameeleza kufurahishwa kwake na uendeshaji wa UDSM Marathon na kusema kuwa inasaidia kufanikisha malengo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuendelea kutoa elimu bora na kuboresha mazingira ya wanafunzi.
Dk Biteko amesema hayo leo Desemba 7 mara baada ya kushiriki mbio hizo za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM MARATHON) zilizofanyika chuoni hapo.

“ Ni dhahiri kwamba mbio hizi zimekuwa muhimu kwa Chuo hiki na jamii kwa ujumla. Tukio hili limeleta pamoja wadau mbalimbali na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia,” amesema Dk Biteko.
Ameongeza “Natambua kwa misimu mitano mbio hizi zimekua zikichangia katika ujenzi wa Kituo cha Wanafunzi kinachojengwa hapa katika Kampasi Kuu ya Mwalimu Nyerere Mlimani. Ujenzi wa kituo hiki ulianza kwa michango kutoka kwa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na washirika mbalimbali wa maendeleo ya elimu ambapo jumla ya shilingi bilioni 4.4 zimechangwa kutoka kwa wadau.”
Aidha, awamu ya kwanza ya ujenzi imekamilishwa kwa kutumia fedha za ndani na hivyo kazi kubwa iliyobaki ni kukamilisha awamu ya pili ili kutimiza ndoto ya kuwa na Kituo cha Wanafunzi kitakachowezesha wanachuo kuwa na maeneo ya kujifunzia na kupata nafasi ya kukuza vipaji vyao.
Ujenzi wa awamu ya pili unahitaji shilingi bilioni 3.3 na hivyo kufanya gharama za ujenzi kwa awamu hiyo kufikia shilingi bilioni 9.4 badala ya shilingi bilioni 6 zilizokadiriwa awali ambazo zimebadilika kwa sababu mbalimbali.



