Tanzania yaadhimisha Uhuru na uchumi imara

TANZANIA leo inaadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara ikiwa na uchumi imara.

Wakati akiwasiliasha mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisema viashiria vya uchumi kwa nusu ya kwanza ya mwaka huu vinaonesha uchumi umeendelea kuimarika.

Alitaja sababu za mafanikio hayo ni jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ya awamu ya sita za kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara na kuimarisha sekta za uzalishaji na huduma za jamii.

Dk Mwigulu alisema Pato halisi la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 5.1 mwaka jana ikilinganishwa na asilimia 4.7 mwaka 2022 na unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.4 mwaka huu.

Ukuaji huo ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kilimo, ujenzi na uchimbaji madini.

Alisema Pato la Taifa linatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 5.8 mwakani na asilimia 6.1 mwaka 2026.

Mwigulu alisema ukuaji huo utategemea utekelezaji endelevu wa miradi ya kimkakati inayohusisha miundombinu ya nishati na usafirishaji, kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi, jitihada za serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara.

Pia, Dk Mwigulu alisema ukuaji huo utategemea utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili – ASDP II, utekelezaji wa mapendekezo na Mkakati wa Tume ya Haki Jinai, uwepo wa utawala bora pamoja na uwekezaji wa serikali katika sekta za huduma za jamii.

Wakati wa kikao cha kujadili utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Kupunguza Umasikini nchini (PSSSN IIl) alisema hali ya umasikini nchini ilipungua kutoka asilimia 28.4 kwa mwaka 2011 na kufikia asilimia 26.2 katika mwaka 2017.

Hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo akiwa katika mkutano na wahariri wa habari Dar es Salaam alisema mwaka 2000 pato la taifa lilikuwa Sh trilioni 33.7 (Dola za Marekani bilioni 13) na sasa pato la taifa ni Sh trilioni 207.9 (Dola za Marekani bilioni 80) ukiwa ni ukuaji wa takribani mara tano.

Alisema pato la mtu mmoja mmoja Tanzania mwaka 2000 lilikuwa Sh 998,385 (Dola za Marekani 384) na kuwa kwa taarifa za Benki ya Dunia za hivi karibuni pato la mtu mmoja mmoja ni Sh 3,145,954 (Dola za Marekani 1,210) ukiwa ukuaji wa takribani mara nne.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (REPOA) Dk Donald Mmari alisema Tanzania imepiga hatua ikilinganishwa na kipindi Tanganyika ilipopata Uhuru.

Dk Mmari alisema kiwango cha umasikini kimepungua na kwa mujibu wa utafiti wa pato la matumizi ya kaya miaka ya 1990 karibu asilimia 50 walionekana kuwa masikini.

“Kile kiwango kimeshuka hadi kwenye asilimia 26, kwa hiyo tumepiga hatua kubwa lakini hatuwezi kusema kuwa tumefika tulipotaka, Mwalimu alitaka kusiwe na umasikini kabisa kusiwe na masikini hata mmoja watu wote wawe shuleni na kusiwe na maradhi lakini changamoto hizo bado zipo,” alisema.

Dk Mmari alisema pamoja na mafanikio hayo bado mfumo wa uchumi haujabadilika kwa kiwango kikubwa na kwa sababu takribani asilimia 65 ya watu wanategemea sekta ya kilimo.

“Serikali ina wajibu wa kuendelea kuweka sera bora na mazingira rahisi ya kufanya biashara na kushiriki katika shughuli za kiuchumi bila kukutana na vikwazo, inapaswa pia kuangalia mfumo ambao wananchi wanaweza kupata mitaji na teknolojia kwa njia rahisi ikawawezesha kukuza tija katika sekta mbalimbali,” alisema.

Dk Mmari alipongeza mafanikio katika sekta ya elimu na akasema wakati wa Uhuru Watanzania waliosoma vyuo vikuu walikuwa wachache na hakukuwa na wasomi wanaoendesha taasisi.

“Kwenye eneo hilo tumepiga hatua kubwa sana sasa tuna vyuo vikuu vingi vinachukua wanafunzi wengi na shule za msingi na sekondari nyingi, tuna asilimia kubwa ya watoto wenye umri wa kwenda shule wapo shuleni na kwa kiasi kikubwa pia sekondari,” alisema Dk Mmari.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button