Serikali kurejesha hadhi ya madini ya Tanzanite

WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde amesema Serikali imejidhatiti kurudisha hadhi ya Tanzanite kwa kufanya minada ndani na nje ya nchi ili kuyaongezea thamani na wafanyabiashara waweze kunufaika na kuongeza pato la taifa kwa ujumla.
Waziri Mavunde amesema hayo leo Desemba 14 Mirerani mkoani Manyara wakati akizindua mnada wa madini ya vito ambao mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2017.
Mavunde amesema mojawapo ya maeneo yanayosaidia kuongeza mapato ni pamoja na kudhibiti biashara ya madini, kuzuia utoroshaji na kuifanya biashara hiyo kuwa katika mfumo sahihi, uwepo wa minada utachochea uongezaji thamani ya madini ya vito.
“Madini ya Vito yananunuliwa kwa asilimia kubwa kwa ajili ya ‘luxury’ ni ufahari na madini ya vito tunashindana na watu wengine ndio maana Serikali inaendelea kuchukua hatua, tunarudisha hadhi ya Tanzanite ili ikashindane vizuri duniani,”amesema Waziri Mavunde
Ameongeza: “Moja ya hatua ya kwanza ni urejeshaji wa minada ya ndani na ya kimataifa, ili tuyape thamani madini yetu, duniani kuna madini mengi ya vito, moja ya sifa kubwa ya madini ya vito ni uadimu, Tanzanite ina sifa hizo.”
Mavunde amesema katika vipengele vya mawe duniani, jiwe linaanzia kuwa Precious, semi-Precious halafu baadaye linakuwa jiwe la kawaida na kwamba wanachukua hatua za makusudi ili Tanzanite lisiwe jiwe la kawaida.
“Tukiacha liwe la kawaida mtanunua kwa kilo kwa gharama ndogo sana na mtashusha hadhi ya Tanzanite, Serikali haipo tayari kuona hilo linatokea,” amesisitiza.

Habari Zifananazo

Back to top button