Wanawake washauriwa kujitokeza uongozi

WANAWAKE wamehimizwa umuhimu wa kuendelea kujitokeza kwa wingi katika kuwaniwa nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Lilian Liundi amesema hayo leo katika kusheherekea kongamano la wanawake miaka 30 ya Beijing iliyofanyika Dar es Salaam.

“Wanawake wameitikia na kujitokeza kugombea wamefanikiwa kushika nafasi za wenyeviti anaamini data zitaendelea kuongezeka siku hadi siku,” amesema.

Amesema “Takwimu zinaonesha asilimia 6.5 tu ya wanawake waliochaguliwa kwenye uchaguzi wa 2019 ni madiwani, na kwamba asilimia 2.1 ya wanawake waliochaguliwa Tanzania nzima walishika nafasi ya wenyeviti wa vijiji, 6.7 wenyeviti wa vitongoji na 12.6 wenyeviti wa mtaa, takwimu hizo zikionesha hawajafikia asilimia wanazotazamia.

“Tunayo imani kwamba kuna uchaguzi wa mwaka ujao data zitakuwa tofauti lakini hapa tunayo mifano ya wanawake waliopasua miamba kwenye uchaguzi uliopita,”amesema Lilian.

Kwa upande wake Rais wa kwanza wa Bunge la Afrika Getrude Mongella ambaye pia, aliteuliwa Katibu Mkuu wa Beijing amesema kuelekea katika uchaguzi mkuu ujao wagombee wanawake watafutwe walio sahihi.

“Tutafute watu sahihi, tuwape moyo ili mwakani hiyo asilimia kubwa tunayoitafuta tuwe nao. Na pia tuendelee kutoa michango ya mawazo na vitendo na kujitolea katika kuhakikisha tunakamilisha hayo mapinduzi,”amesema.

Amesema kazi hiyo sio nyepesi inahitaji kujengwa katika dira ya miaka 50 ili hatua zifuatwe taratibu na kuwe na kupokezana vijiti baada ya muda fulani.

Mwenyekiti wa Bodi wa TGNP Gemma Akilimali amesema ana furaha kubwa kwa kuwa kongamano lao limefanyika baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa  ambap mwaka huu wanawake wamepata hamasa kubwa ya kushiriki katika kinyang’anyiro cha uchaguzi.

Amesema pamoja na changamoto mbalimbali lakini wapo wengi waliopata uongozi, kuna maeneo ambayo wanawake wameshika nafasi ya wenyeviti wa serikali za mitaa kwa mara ya kwanza

“Hili ni jambo la kujivunia na kusherehea. Tukumbuke kuwa 2025 tunaadhimisha miaka 30 tangu kufanyike mkutano mkubwa wa wanawake duniani uliofanyika Beijing hivyo, kama sehemu ya kusherehekea leo tupo na wanawake walioshiriki miongoni mwao ni  Zakia Meghji, Ruth Meena, Eda Sanga, Hellen Bisimba na wengine,”amesema

Amesema kongamano hili limelenga kuwaleta wanawake mbalimbali walio katika nafasi mbalimbali za uongozi hususani viongozi wa kisiasa ili waweze kushirikishana uzoefu.

Katika kongamano hilo TGNP iliwapa tuzo wanawake walio na ujasiri na uthubutu Pamoja na kuzindua kitabu cha safari ya Beijing.

Habari Zifananazo

Back to top button