Diarra aiwahi TP Mazembe

KIPA namba moja wa Yanga, Djigui Diarra amerejea kwenye mazoezi ya timu hiyo tayari kwa mchezo wa marudiano hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe.
Kurejea kwa kipa huyo raia wa Mali, ni faraja kwa timu hiyo inayojiandaa na mchezo huo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Jumamosi wiki hii.
Kwenye mchezo wa awali uliochezwa Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Diarra aliyekuwa akisumbuliwa na majeraha, amekosekana kwenye mechi za Yanga Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Fountain Gate ambazo makipa, Abubakary Khomein na Abutwalib Mshery walikaa langoni.
βTunashukuru Mungu baadhi ya wachezaji wetu waliokuwa majeruhi kama kipa wetu chaguo la kwanza, Djigui Diarra ameanza mazoezi kamili na wenzake, sambamba na Maxi Nzengeli. Ni uamuzi wa kocha kama awatumie kwenye mchezo dhidi ya TP Mazembe au la,β alisema Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe jana akielezea afya za wachezaji kwenye kikosi cha timu hiyo jana.
Aidha, Kamwe amewaomba mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi Jumamosi kuiunga mkono timu hiyo kwenye mchezo huo muhimu.
Yanga inashika mkia, ikiwa na pointi moja huku Al Hilal ya Sudan wakiongoza kundi, wakikusanya pointi tisa, MC Alger inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi saba na Mazembe nafasi ya tatu wakikusanya alama mbili.



