CCM Iringa yaelekeza macho Uchaguzi Mkuu

Ushindi wa asilimia 99.99 kilioupata katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Novemba, mwaka jana umekipa matumaini Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa ya kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao wa Rais, wabunge na madiwani.

Ushindi huo wa mitaa umesemekana kuwa ni matokeo ya utekelezaji thabiti wa Ilani ya CCM chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika kikao na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yasin, alieleza kuwa chama kimefanikiwa kuimarisha imani ya wananchi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa mkoani humo.

“Tumefanikisha miradi mikubwa ya miundombinu, elimu, afya, na huduma za kijamii. Ushindi huu ni wa jasho, siyo figisufigisu kama wengine wanavyodai,” alisema na kuongeza kwamba CCM imeshinda vitongoji 1,839 kati ya 1,840, vijiji vyote 360, na mitaa yote 222.

Alisisitiza kuwa maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu yanaendelea kwa kasi, akiwataka wanachama kuendelea kushikamana na kuheshimu miongozo ya chama.

“Tunajiandaa kushinda kwa kishindo tena katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Ushindi wa asilimia 100 uko ndani ya uwezo wetu,” aliongeza.

Mwenyekiti huyo pia alitumia fursa hiyo kuwashukuru waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa kwa kazi yao ya kueneza taarifa za utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa wananchi na akaahidi daraja hilo kutumika kwa nguvu kubwa mwaka huu.

“Waandishi wa habari mmekuwa daraja muhimu kati ya CCM na wananchi. Mmetusaidia kuonyesha kazi za maendeleo na kuongeza imani ya wananchi kwa chama chetu,” alisema Yasin.

Aidha, alionya dhidi ya vitendo vya rushwa na kampeni za mapema miongoni mwa wagombea, akisema chama hicho kimeanza kuchukua hatua na hakitasita kufanya maamuzi magumu dhidi ya wale watakaokiuka taratibu.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa chama akiwemo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Abri Asas, na Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Said Goha.

Asas alisisitiza umuhimu wa mshikamano na ushirikiano kati ya chama na wanahabari katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu masuala ya maendeleo.

Aliongeza juhudi za Rais Samia katika kuleta maendeleo, akisema kuwa utekelezaji wa Ilani umeimarisha imani ya wananchi kwa CCM.

Kwa mujibu wa Asas, CCM itaendelea kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha mahitaji ya wananchi yanapewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo ya chama hicho.

 

Habari Zifananazo

Back to top button