Bobi Wine adai Jen.Kainerugaba anapanga kumkamata

UGANDA : KIONGOZI wa upinzani nchini Uganda, Bobi WIne amedai kuwa Muu wa Jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, anajipanga kutaka kumkamata.
Kwa mujibu wa chapisho aliloweka kwenye X (zamani Twitter) Jumapili jioni, Kainerugaba, ambaye ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, alisema kwamba babake, ambaye ameiongoza Uganda tangu mwaka 1986, ndiye mtu pekee anayemlinda dhidi ya mwanasiasa huyo.
Bobi Wine, ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2021, alijibu kauli hiyo akisema kuwa vitisho vya mtoto wa rais anavichukulia kwa uzito kutokana na hofu ya kuuawa.
Bobi, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, alieleza kuwa serikali ya Uganda inatishia maisha ya wafuasi wake. SOMA: Serikali ya Uganda yajitenga na ‘utashi’ wa mtoto wa Museveni
Hata hivyo, msemaji wa wanajeshi nchini Uganda alikataa kutoa maoni kuhusu suala hili, akieleza kuwa kauli za Kainerugaba kwenye mitandao ya kijamii zinapaswa kuchukuliwa kama “stihizai” na haziwezi kuhusishwa na sera za serikali ya Uganda.
Bobi Wine, ambaye awali alikuwa mwanamuziki maarufu kabla ya kuingia kwenye siasa, ameendelea kupinga vikali madai ya serikali kwamba alihongwa na serikali ya Uganda katika shughuli zake za kuwania urais.
“Iwapo walinifadhili, kwanini wananifuata kila mahali na kuua wafuasi wangu?” alihoji.
Katika uchaguzi wa 2021, Bobi Wine alikataa matokeo ya uchaguzi, akidai kuwa ulifanyika wizi wa kura na wapiga kura walitishiwa maisha ili kuhakikisha ushindi wa Museveni.



