Serikali ya Uganda yajitenga na ‘utashi’ wa mtoto wa Museveni
UGANDA imejitenga na kauli za mtandaoni za mtoto wa Rais Yoweri Museveni, Muhoozi Kainerugaba kuhusu uwezo wake kuiteka Nairobi ndani ya wiki mbili, ikisema nchi hiyo imejitolea kuishi pamoja kwa amani na Kenya.
Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda ilisema Jumanne kwamba imebainisha mjadala unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Kenya na jirani yake Uganda na kwamba inathamini uhusiano mkubwa wa nchi hizo mbili.
“Wizara inapenda kusisitiza kwamba Serikali na watu wa Jamhuri ya Uganda wanathamini uhusiano thabiti uliopo kati ya watu na Serikali ya Jamhuri ya Kenya kwa kuzingatia historia yetu ya pamoja, maadili ya pamoja, kuheshimiana, kuaminiana na nia yetu. ili kujenga jumuiya yenye umoja ya Afrika Mashariki,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
“Kwa maana hii, Serikali ya Jamhuri ya Uganda ilitaka kusisitiza ahadi yake ya ujirani mwema, kuishi pamoja kwa amani na ushirikiano,” iliongeza taarifa hiyo.
Hata hivyo muda mchache taarifa ilitoka kuwa Rais Museveni amempandisha cheyo cha kijeshi Muhoozi kutoka Luteni Jenerali hadi Jenerali hata hivyo amemfuta kazi kama Mkuu wa Majeshi ya Nchi Kavu.
Promotions And Appointments In UPDF https://t.co/lKjo373iv9 pic.twitter.com/LhQ9krNJdQ
— Defence Spokesperson (@UPDFspokespersn) October 4, 2022
Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Jeshi ilisema Rais Museveni amempandisha Cheyo Kayanja Muhunga kuwa Luteni Jenerali na pia kumteua kuwa Mkuu wa Majeshi ya Nchi Kavu huku Jenerali Muhoozi akiendelea kusalia kama Mshauri Mkuu wa Rais Operesheni Maalum.
Jenerali Muhoozi aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba alihitaji wiki mbili tu kuichukua Nairobi, Kenya.
Tweet ya Jen. Muhoozi ilitishia kuibua mtafaruku wa kidiplomasia kwa nchi hizo mbili jirani.
Kwa mujibu wa tweet, Jen. Muhoozi alianza kwa kumlaumu Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ambaye anamtaja kama kakake mkubwa kwa kutowania muhula wa tatu katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8, 2022.
Aliandika, Rais mstaafu Kenyatta angeweza kushinda uchaguzi huo kwa urahisi.
“Tatizo langu pekee na kaka yangu mkubwa ni kwamba hakugombea muhula wa tatu. Tungeshinda kirahisi,” aliandika kwenye Twitter.
Hata hivyo, hili halingewezekana kwani katiba ya Kenya inaruhusu Mkuu wa Nchi kuhudumu kwa mihula miwili pekee.
Muhoozi usiku wa Jumatatu, Oktoba 3, 2022, aliendelea na kusema kwamba nchi hizo mbili zinafaa kufanya kazi pamoja lakini Wakenya hawakushawishika.
“KOT, nawasamehe wote kwa matusi mliyonitusi. Tafadhali tushirikiane kuifanya Afrika Mashariki kuwa kubwa!” aliendelea kuandika.
Union is a MUST! No honourable men can allow these artificial, colonial borders anymore. If we our generation has men then these borders must fall! pic.twitter.com/60E9nzKIqI
— Muhoozi Kainerugaba (@mkainerugaba) October 4, 2022
Wizara ilisema kuwa Serikali ya Uganda haifanyi Sera yake ya Mambo ya Nje na shughuli nyingine rasmi kupitia mitandao ya kijamii wala haitegemei vyanzo vya mitandao ya kijamii katika kushughulikia serikali nyingine huru.
Aidha ilikariri kuwa uhusiano wa kindugu kati ya mataifa hayo mawili bado upo na kuwahakikishia Wakenya kuwa mambo yote yalikuwa sawa.
Saa chache baada ya Waziri anayeshughulikia Masuala ya Kigeni wa Kenya Alfred Mutua kufanya mkutano na Kamishna Mkuu wa Uganda nchini Kenya, Balozi Dk Hassan Galiwango, aliwahakikishia Wakenya kwamba hakuna sababu ya kutisha.
“Leo asubuhi nilishiriki kikombe cha chai cha kijamii na Amb. Dk Hassan Galiwango – Kamishna Mkuu wa Uganda nchini Kenya. Tulijadili mambo ya kuvutia. Mambo iko Sawa,” Dk. Mutua alisema.
Baadaye, Jenerali Muhoozi alikariri na kusema kwamba maoni hayo yalikuwa ni mzaha tu.
Pia alisema nchi hizo mbili jirani bado zinaendelea na azma ya kuunganisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Union is a MUST! No honourable men can allow these artificial, colonial borders anymore. If we our generation has men then these borders must fall! pic.twitter.com/60E9nzKIqI
— Muhoozi Kainerugaba (@mkainerugaba) October 4, 2022
“Muungano ni lazima. Hakuna watu wa heshima wanaoweza kuruhusu mipaka hii ya bandia, ya kikoloni tena. Ikiwa kizazi chetu kina wanaume basi mipaka hii lazima ianguke,” Jenerali Muhoozi alidai.
Aliendelea kueleza kuwa baada ya kuundwa kwa umoja huo, babake Rais Yoweri Kaguta Museveni ndiye atakuwa rais.
“Baada ya kuunda Shirikisho letu la Afrika Mashariki. Rais Museveni atakuwa Rais, Afande Ruto atakuwa Makamu wa Rais, ndugu yangu Uhuru atakuwa Waziri wa Mambo ya Nje. Nataka tu kuwa CDF wa majeshi ya Afrika Mashariki.”