M23 kuwaponza Waandishi wa Habari DRC
WAZIRI wa Sheria wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Constant Mutamba, ametangaza kuwa waandishi wa habari nchini humo watakabiliwa na adhabu ya kifo kwa kuripoti shughuli za kundi la waasi la M23.
Kwa mujibu wa ripoti ya tovuti ya DRC News leo, Waziri amesema, “Mtu yeyote wa kisiasa au wa asasi za kiraia, mwandishi wa habari, au kiongozi wa kidini atakayetoa taarifa kuhusu shughuli za jeshi la Rwanda na kundi la M23, sasa atakabiliwa na adhabu kali ya kisheria (ADHABU YA KIFO).”
Tayari kituo cha televisheni cha Al Jazeera, kimekumbwa na adhabu ya Serikali ya DR Congo ya kufutiwa uhalali wake nchini humo kufuatia mahojiano na Rais wa M23, Bertrand Bisimwa.
Baada ya hatua hiyo dhidi ya Al Jazeera, DRC imetoa onyo kwa vyombo vya Habari vya RFI, France 24 na TV5.
DRC imesema itatumia nguvu kamili ya sheria dhidi ya vyombo vya habari vinavyoonekana kuunga mkono kundi la M23.



