Obasanjo afanya ibada kumuombea Carter

NIGERIA : RAIS wa zamani wa Nigeria, Chifu Olusegun Obasanjo, amefanya ibada ya ukumbusho huko Abeokuta, Kusini Magharibi mwa Nigeria, kwa heshima ya Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter, ambaye alifariki dunia Desemba 29, 2024, na kuzikwa wiki iliyopita.

Akiongea kwa huzuni, Obasanjo, ambaye alimtaja Carter kama rafiki yake wa karibu, alisema atamkosa sana lakini aliongeza kuwa ana imani kuwa wataonana tena peponi. “Nitammiss sana lakini najua tutakutana tena peponi,” alisisitiza.

SOMA: Obasanjo avishwa nishani ya heshima

Obasanjo alimtaja Carter kama mtu mwadilifu ambaye alijitolea kwa nguvu zake zote katika harakati za ukombozi wa Afrika dhidi ya utawala wa kibeberu na ubaguzi wa rangi, hasa katika bara la Afrika Kusini. Alisema, “Jimmy Carter alikuwa mtu aliyetetea haki za binadamu na usawa wa watu wote duniani.”

Akizungumzia ukaribu wao kama marafiki na viongozi walio na ajenda ya pamoja, Obasanjo alikiri kwamba Carter ndiye aliyemsaidia kuishi hadi leo. “Yeye ndiye sababu ya mimi kuwa hai leo,” alisema Obasanjo kwa huzuni.

Aidha, Obasanjo alielezea kuwa Nigeria, Afrika, na dunia kwa ujumla imepoteza rafiki na mshiriki ambaye alifanya kazi kwa bidii na kwa ridhaa katika kuhimiza amani na ustawi wa kimataifa.

Jimmy Carter alikua Rais wa kwanza wa Marekani kutembelea Nigeria, ambapo alifika kutoka Brazil Machi 31, 1978. Ziara hiyo ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa sababu ilikuwa kipindi cha vita vya Nigeria dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini, huku Nigeria ikichukua jukumu muhimu katika harakati za ukombozi barani Afrika, akisaidia nchi kama Angola, Namibia, Zimbabwe, na Msumbiji kwa rasilimali na msaada wa kijeshi.

Habari Zifananazo

Back to top button