DED wa zamani Simanjiro mbaroni uhujumu uchumi

MAHAKAMA ya  Wilaya  ya Simanjiro mkoani Manyara imemshikilia aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Samwel Warioba Gunzar kwa makosa mawili  ya uhujumu uchumi.

Makosa hayo ni  matumizi mabaya ya madaraka na kosa la pili la kutotimiza wajibu wa kisheria ambapo ni kinyume cha sheria.

Akisoma shauri hilo Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Simanjiro,Wakili Faustin Mushi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi Wilaya ya Simanjiro, Charles Uisso alisema mshtakiwa katika nyakati tofauti akiwa Mkurugenzi  wa halmashauri hiyo alitoa zabuni ya ukusanyaji wa mapato ya soko la mnada wa Orkesumet kwa mwananchi aitwaye Elias Lazaro Tipiliti bila ya kuwepo kwa tangazo la zabuni na bila ya zabuni hiyo kushindanishwa.

Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka Faustin Mushi mahakamani hapo amesema kwamba mshtakiwa amefunguliwa shauri Na.ECC.1048/2025 kwa makosa mawili.

Kosa la kwanza amesema ni la matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022 ikisomwa pamoja na Aya ya 21 jedwali la 1 kifungu cha 57(1) na 60(2) vya sheria ya uhujumu uchumi na makosa ya kupanga sura 200 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Aidha mshtakiwa ameshtakiwa kwa kosa la pili la kutotimiza wajibu wa kisheria kinyume na kifungu cha 123 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Amebainisha kwamba mshtakiwa amekana makosa yote mawili na yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana kwa kupeleka wadhamini wawili ambao ni watumishi wa umma pamoja na vitambulisho  vyao pamoja na kusaini bondi ya million mbili.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa tena Februari 11, 2025 kwa ajili ya kusikilizwa mashahidi wa upande wa Jamuhuri.

Habari Zifananazo

Back to top button